Sunday, December 30, 2007

BREAKING NEWS-UCHAGUZI KENYA

Tume ya uchaguzi ya Kenya hivi punde imemtangaza Mwai Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais. Raila Odinga ameshika nafasi ya pili na Kalonzo Musyoka nafasi ya tatu.
Kwa mujibu wa ECK, Kibaki wa PNU ameshinda jumla ya kura 4,584, 721 akifuatiwa na Raila Odinga ODM aliyepata kura 4,352,993 na Musyoka wa ODM-Kenya ambaye amepata kura 879, 903.
Lakini habari za kiiteligensia zinadai kuwa yameandaliwa machafuko makubwa nchini humo na kuna uwezekano hali ya hatari ikatangazwa

Raila Alonga

Mgombea wa ODM, Raila Odinga, ameitisha mkutano waandishi wa habari asubuhi hii na kuitaka tume ya uchaguzi (ECK) kuacha kutangaza matokeo ambayo anadai yamepikwa.

Katika mkutano huo, Raila aalimtaka mwenyekiti wa tume hiyo, Samuel Kivuitu, kujiuzulu wadhifa wake kuliko kukubali kutumika kumuweka mtu madarakani kwa hila.

Lakini inashangaza kuwa raila amesema hawezi kwenda mahakamani kupinga yale anayoyaona kuwa ni kasoro. Anataka kufanya nini?

Raila anaamini kuwa matokeo ya baadhi ya maeneo yalifichwa makusudi ili kuokoa kahazi kwa rais Mwai Kibaki katika mazingira kama yaliyotokea.

Aliyataja baadhi ya majimbo ambayo yalificha matokeo kwa ajili hiyo kuwa ni Juja, Nithi, Maragua, Kiambaa na Gatanga, ambayo yana wafuasi wengi wanaomuunga mkono Kibaki.

Pia kuna tofauti kubwa kati ya idadi ya kura zilizotangazwa na ECK na matokeo ambayo ODM imeyapata kutoka kwa wasimamizi wake katika baadhi ya vituo. Akitoa mfano, raila alisema ECK inasema huko Juja, Kibaki amepata kura 78,000 wakati mawakala wa ODM wanaonyesha kuwa kura aliziopata Kibaki ni 52,000 tu.

Pia matokeo ya ECK yanaonyesha kuwa katika baadhi ya vituo, idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ni zaidi ya asilimia 100 ya watu waliojiandikisha.

Raila sasa anaitaka ECK kupitia upya, matokeo yote iliyoyatangaza. Mpaka kazi ya kutangaza matokeo inasitishwa jana jioni, takwimu za ECK zilikuwa zikionyesha kuwa raila alikuwa anaongoza kwa kura 3,880,053 dhidi ya kura 3,842,051 za Kibaki.

Saturday, December 29, 2007

ECK Yasitisha Matokeo

Hatimaye ECK imelazimika kusimamisha zoezi la kujumlisha na kutangaza matokeo baada ya ODM kulalamika kuhusu matokeo ya majimbo 10. ODM imetaka kwanza ifanyike kazi ya kuhakiki kura katika majimbo hayo kabla kazi ya kujumlisha na kutangaza matokeo haijaendelea. Inasemekana katika moja ya majimbo hayo, walijiandikisha watu 60,000 lakini matokeo yanaonyesha kuwa Kibaki pekee ana kura zaidi ya 80,000!

MAMBO YABADILIKA KENYA

Mambo yanaonekana kubadilika sana jioni hii katika mato9keo ya uchaguzi Kenya. Mtiririko wa matokeo ulikuwa unaonyesha kuwa upinzani unashinda, lakini takwimu za jioni hii zimebadilisha matokeo kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa ECK, Raila bado anaongoza kwa tofauti ndogo sana na kura. Mpaka sasa amepata kura 3,880,053 huku Kibaki akifuatia kwa karibu akiwa na kura 3,842,051. Nadhani Musyoka ameamua kukubali yaishe kwa sababu hakuna hata anayemtaja

MATOKEO HADI SASA

hadi mchana huu, matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) yanaonyesha kuwa bado raila anaongoza kwa kuwa na kura 4,356,092 akifuatiwa na Kibaki mwenye kura 4,009,300 na Musyoka ameambulia kura 452,952.
Kwenye ubunge, chama cha raila cha ODM kimejinyakulia viti 70 wakati PNU cha Kibaki kina viti 24 na ODM-K ya Musyoka ina viti 9.
Matokeo haya yanahusisha majimbo 189 kati ya majimbo 210, kwa maana hiyo bado matokeo ya majimbo 21 tu.

HII NI IDADI YA KURA HADI LEO ASUBUHI

KIBAKI ODINGA MUSYOKA
Nairobi 159,959 192,843 24,995
Eastern 178,422 35,919 360,470
Nyanza 110,169 1,097,085 1,992
Coast 100,456 176,734 17,812
Central 1,139,127 14,447 6,458
North Eastern 60,245 55,674 5,392
Western 237,535 587,731 6,074
Rift Valley 499,639 1,216,322 32,453
Total 2,485,552 3,376,755 455,646

MATOKEO KENYA

Mpaka asubuhi ya leo (Desemba 29), raila odinga alikuwa anaongoza kwa takribani kura milioni moja katika kinyang’anyiro cha urais wa Kenya.

Matokeo kutoka katika majimbo 112 kati ya majimbo 210, ambayo ni zaidi ya nusu ya majimbo yote, yanaonyesha kuwa Raila anaongoza kwa kupata kura 3, 268,571 dhidi ya kura 2,278,355 za rais Kibaki. Kalonzo Musyoka wa ODM-Kenya yeye amejipatia kura 356,632.

Inavyoonekana hata kama muujiza utatokea na Kibaki akashinda, serikali yake haiwezi kufanya kazi ipasavyo kwani matokeo yanaonyesha kuwa Raila na ODM yake watakuwa na viti vingi Bungeni.

Mkapa wakati huu, Raila na chama chake walikuwa wanakaribia kupata viti 80 wakati PNU ikijikongoja kwa viti ambayo haviki hata 20. Mbaya zaidi timu kubwa ya mawaziri ambao Kibaki alikuwa akiwategemea kuwa watarudi Bungeni imeshindwa akiwemo makamu wake, Moody Awori.

KANU ndiyo inaelekea kufa kwani hata watoto wa Moi waliokuwa wakitarajiwa kuwa ndio wangekuwa wakombozi, wote wamepigwa chini.

Endelea kufuatilia matokeo hayo kupitia hapa kwani nitakuwa nikiyahuisha kila taarifa mpya zitakapotolewa.

Thursday, December 27, 2007

Polisi na Magereza wameanza tena kuua wahalifu?

KWA muda wa wiki takriban mbili sasa kumekuwa na taarifa ambazo zinatia madoa taasisi mbili muhimu nchini; jeshi la Polisi pamoja na Magereza. Taarifa hizo zinahusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa dhidi ya watu ambao wapo chini ya himaya ya ulinzi wa taasisi hizo.

Katika moja ya taarifa hizo, inadaiwa kuwa mtu aliyekamatwa kwa tuhuma za mauaji ya mkewe huko Mwanza, alipigwa na askari akiwa katika kituo cha polisi na kufariki dunia.

Kwa upande mmoja, askari wanaotuhumiwa kufanya hivyo wamekanusha na kutoa taarifa kuwa mtu huyo alifariki akiwa hospitali kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa wananchi wenye hasira kabla hajakamatwa na askari hao.

Lakini kwa upande mwingine, mashuhudaa, akiwamo kiongozi wa serikali ya mtaa, wanasema kuwa mtu huyo hakupigwa na wananchi wenye hasira kama askari wanavyoeleza.

Maelezo ya mashuhuda wengine ambao ni au walikuwa mahabusu katika kituo ambacho marehemu alipelekwa, wanadai kuweko kwa tukio la mtuhumiwa huyo kupigwa na askari na kufariki akiwa kituoni hapo.

Kutoka Kibaha kuna taarifa nyingine za mtuhumiwa kufariki akiwa mikononi mwa Polisi. Kama inavyodaiwa kutokea Mwanza, mtuhumiwa huyu naye anadaiwa kufariki kutokana na kipigo cha askari ambao kimsingi walipaswa kumlinda asidhurike.

Kama kawaida, askari polisi wamekanusha kuhusika na kifo hicho wakidai kuwa walimfikisha mtuhumiwa hospitali akiwa mahututi. Lakini maofisa wa hospitali nao wanakana kuhusika na kifo hicho wakisema kuwa mtu huyo alifikishwa kwao akiwa tayari ameshafariki dunia.

Kutoka Singida Jeshi la Magereza limejikuta katika wakati mgumu na kuingia lawamani kwa madai kuwa lilishindwa kumpatia huduma za matibabu ya haraka mfungwa mmoja aliyekuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha 10 gerezani kwa kosa la unyang’anyi.

Inaelezwa kuwa mfugwa huyo alipigwa na askari hadi kuvunjika kiuno na mgongo alipokuwa akifanya kazi kwenye gereza wilayani Iramba.

Inadaiwa kuwa baada ya kupigwa, mfungwa huyo aliachwa kwa muda wa mwaka mmoja bila kupewa matibabu yanayostahili, hali iliyomsababishia kupooza.

Kwa upande wake, Jeshi la Magereza mkoani Singida linaeleza kuwa mfungwa huyo alitumbukia kwenye shimo na kuvunjika mguu na kiuno wakati alipokuwa anafukuzwa na wafungwa wenzake katika harakati za kutoroka.

Lakini haijaelezwa wazi kwa nini mfungwa huyo aliachwa bila matibabhu yanayostahili kwa muda wa mwaka mmoja, licha ya haja ya kupatiwa matibabu hayo kuelezwa na daktari aliyemchunguza baada ya kuumia.

Inavyofahamika ni kuwa hata kama mfungwa huyo aliumia wakati anatoroka, bado anayo haki na anastahili kupatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata na hatimaye ashtakiwe kwa kosa analodaiwa kulifanya.

Matukio haya si ya kwanza ya aina hii kuripotiwa dhidi ya Jeshi la Polisi na Magereza. Lakini kwa kipindi sasa habari zinazofanana na hizi zilianza kupotea na kutuaminisha kuwa taasisi hizo mbili zilikuwa zimeanza kubadilika na kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

Kuibuka upya kwa taarifa hizi, ingawa bado hakuna uthibitisho kuwa yaliyotokea yamesababishwa na watendaji katika taasisi hizo, kunastahili kufanyiwa tathimini ya kina.

Ni mapema mno kuvilaumu vyombo hivi lakini matukio haya yanatulazimisha kuanza kuhoji iwapo taasisi hizi zimeanza tena mchezo wa kuwaua wahalifu?

Sunday, December 23, 2007

Deni la Taifa Laongezeka

Rais Jakaya Kikwete anasema kuwa haelewi nini kinasababisha mfumko wa bei, tujiandae sasa kwani kuna uwezekano akaja na sababu kama hiyo atakapotakiwa kueleza kwa nini deni la taifa linaongezeka.

Ripoti ya Benki Kuu inaonyesha deni la jumla la Taifa liliongezeka mwezi Oktoba na kufikia dola za Marekani milioni 6,894 kutoka kiasi cha dola za Marekani milioni 6,453.5 mwezi uliotangulia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya hali ya uchumi iliyowekwa kwenye tovuti ya BoT hivi majuzi, hilo ni ongezeko la dola za Marekani milioni 440.5, sawa na asilimia 6.8.

Ongezeko hilo linatokana na madeni mapya, kubadilika kwa viwango vya ubadilishaji fedha na limbikizo la riba katika madeni ya nje.

Ripoti hiyo inabainish apia kuwa katika deni hilo, asilimia 76.6 ni deni la nje na asilimia 23.4 ni deni la ndani.

Deni la nje limeongezeka kwa asilimia 6.8 na kufikia dola za Marekani milioni 4,940.4. katika kiasi hicho, dola milioni 4,010.2 zilikuwa ni deni halisi wakati dola milioni 1,268.2, sawa na asilimia 18.4 ya deni lote, lilitokana na malimbikizo ya riba.

Orodha ya taasisi za serikali zilizo madeni inaonyesha kuwa Serikali Kuu ndiyo inayoongoza kwa kuwa na deni linalofikia dola milioni 3,192.4 sawa na asilimia 79.6 ya deni lote ikifuatiwa na sekta binafsi ambayo inadaiwa dola milioni 647 (asilimia 16.1) na taasisi za umma zinadaiwa dola milioni 170.8 sawa na asilimia 4.3.

Ripoti hiyo inaionyesha kuwa katika mwezi huo, malipo ya madeni ya nje yalifikia dola milioni 3.8. kati ya kiasi hicho, dola milioni 2.2 zilikuwa malipo ya madeni halisi na dola milioni 1.6 zilikuwa ni malipo ya malimbikizo ya riba.

Kuhusu deni la ndani, ripoti hiyo inabainisha kuwa nalo liliongezeka na kufikia sh bilioni 1,885.3 ilipofika mwisho wa Oktoba, 2007 ikilinganishwa na deni la sh bilioni 1,860.8
lililorekodiwa mwezi mmoja kabla.

Katika kiasi hiki, dhamana za serikali zilikuwa ni asilimia 99.6 ya deni lote huku taarifa ikionyesha kuwa mabenki ya biashara ndio wakopeshaji wakubwa kwa serikali kwa kuikopesha asilimia 43.7 ya deni lote.

Kuhusu mfumko wa bei, taarifa hiyo inabainisha kuwa ulishuka na kufikia asilimia 7.1 mwezi Oktoba ikilinganishwa na asilimia 8.3 iliyorekodiwa mwezi Septemba.

Wednesday, December 12, 2007

Hujuma Madini

KAMPUNI nyingi za uchimbaji madini nchini zimebainika ‘kukarabati’ hesabu zao kwa kuongeza matumizi yasiyohusika, hivyo kufanya hesabu zao zionyeshe kuwa hazistahili kulipa kodi.

Hayo yamebainishwa katika ripoti iliyoandaliwa na iliyokuwa Kamati ya kupitia mikataba ya madini iliyoongozwa na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Lawrence Masha.

Ripoti hiyo, ambayo ni moja ya ripoti kadhaa zilizotokana na shinikizo kuhusiana na uwezekano wa wawekezaji katika sekta hiyo kuiibia serikali, inaeleza kuwa ujanja unaofanywa na kampuni hizo unahusisha kuingiza katika mahesabu yao hata fedha zinazotumika katika kugharamia miradi ya kijamii.

Kwa maana hiyo, hesabu za kampuni hizo zinaonyesha kuwa mitaji iliyotumika kwa mwaka husika ni mikubwa na haijarejeshwa ili kuiwezesha kampuni kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa makampuni mengi yamekuwa yakiidanganya serikali kuhusu hesabu zao kwa kutumia kipengele cha kusaidia jamii, kwani pamoja na sheria kuwataka watoe msaada kwa maeneo ambayo wanafanya shughuli zao, wao wamekuwa wakijumuisha misaada hiyo katika hesabu zao.

Matokeo yake, hesabu za matumizi ya mtaji za makampuni hayo zinaonyesha wanatumia fedha nyingi na hivyo kuonyesha kuwa kampuni zinapata hasara na hazijafikia sifa ya kulipa kodi.

Ripoti hiyo inabainisha pia kuwa baadhi ya gharama zinazotajwa kama kusaidia jamii, hazihusiani moja kwa moja na miradi ya jamii na kutoa mfano wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda kwenye mgodi unahesabiwa kama msaada kwa jamii wakati kinachofanyika ni kuweka mabomba machache ya kuwapatia maji wananchi katika vijiji linamopita bomba hilo, lakini lengo lake kuu ni kuupatia mgodi maji na si wanavijiji.

Aidha, ripoti hiyo yenye kurasa 33, inayaainisha baadhi ya maeneo ambayo serikali inapoteza mapato kuwa ni pamoja na mahesabu ya kampuni za madini nchini, utoroshaji wa fedha nje ya nchi, manunuzi pamoja na ujanja unaofanywa na baadhi ya kampuni kuiweka migodi yao tofauti chini ya umiliki mmoja.

Kwa kiasi kikubwa, ripoti hiyo inasema kuwa serikali inapotea mapato hayo kutokana na udhaifu wa mikataba pamoja na taasisi zake, ikiwamo Wizara ya Nishati na Madini yenyewe, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na taasisi nyingine zionazohusika na kuratibu sekta hiyo.

Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa mikataba, wawekezaji katika sekta hiyo wapo huru kusafirisha mazao wanayozalisha nje ya nchi.

“Ukiondoa mkataba wa Bulyanhulu, mikataba mingine haina vipengele kuhusu utaratibu wa masoko. Kipengele hiki ni muhimu kwa sababu kinaweka uwazi katika masuala ya bei,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ikifafanua, ripoti hiyo inabainisha kuwa wawekezaji wengi katika sekta hiyo wamekuwa wakiwasiliana na mawakala wanaosafisha madini nje ya nchi na wakishayapeleka madini ghafi, yakishasafishwa huuzwa huko huko bila serikali kuwa na habari ya kiasi cha madini yaliyouzwa.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo ilipendekeza kufanyiwa marekebisho kwa kanuni za uchimbaji madini za mwaka 1999 ili kuweka kipengele kitakachozilazimisha kampuni za madini kutoa kwa serikali mikataba yao ya wanunuzi wa madini.

Kwenye masuala ya kodi, ripoti hiyo inaonyesha kuwa kampuni nyingi zinatumia ujanja katika mahesabu yake kiasi kwamba kwa miaka mingi yanaonekana kutopata faida na hivyo kutolipa kodi.

Kwa mujibu wa mikataba mingi hapa nchini, kampuni za madini za madini haziwezi kutozwa kodi hadi hesabu zake zionyeshe kuwa zimerejesha mitaji yake kwa asilimia 100.

Baada ya kuonyesha mifano kadhaa ya nchi ambazo hazifuati mtindo huo, kamati hiyo inabainisha kuwa kuacha kampuni irudishe mtaji wake kwa asilimia 100 kunaigharimu nchi na pia kunapingana na taratibu za kodi zilizoainishwa katika kifungu cha 17 cha sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 2004.

Kamati inasema kuwa upendeleo huo wa kurudisha mtaji unatoa mwanya kwa kampuni hizo kupanga hesabu na kuonyesha kuwa hawajarudisha gharama za mitaji na jambo hilo limeinyima serikali kodi tangu uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini uanze nchini.

Ripoti inasema kuwa ukichanganya na utaratibu wa kampuni kujumuisha migodi yake yote katika hesabu za pamoja, utaratibu huu unazidisha kuonyesha jinsi kampuni hizo zisivyopata faida kwani uwekezaji mkubwa katika mgodi mmoja unaweza kunyonya faida inayopatikana katika mgodi mwingine na kampuni kuonekana haijapata faida.

Kuhusu utoroshaji wa fedha nje ya nchi, ripoti hiyo inabainisha kuwa mikataba ya madini inayataka makampuni kupata ruhusa na Benki Kuu (BoT) kufungua akaunti nje ya nchi ili kuwezesha kuweka fedha zinazopatikana nje, hasa mikopo.

Ruhusa hiyo ya BoT inatolewa kwa masharti kuwa ipatiwe taarifa za benki kila mwezi na akaunti hizo zifungwe mara baada ya deni kumalizika kulipwa.

“Imeripotiwa kwa makampuni mengi hayazingatii masharti haya hasa kutoa ripoti za benki za kila mwezi. Pia makampuni mengi yanapokea fedha nyingi bila dhamana kutoka kwa kampuni zao mama na wanahisa wake bila ya kupata ruhusa rasmi kutoka BoT,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kamati hiyo iliishauri Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na BoT, kufanya uchunguzi wa usafirishaji huu wa fedha.

Kuhusu suala la uajiri na mafunzo kwa wazalendo, ripoti hiyo inabainisha kuwa kampuni nyingi haziwasilishi serikali mipango yake ya uajiri na mafunzo kwa wazalendo licha ya kutakiwa kufanya hivyo kupitia sheria ya madini ya mwaka 1998.

Hiyo imeonyesha kukinzana kwa sheria ya uhamiaji ya mwaka 1995, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1997 ambayo inasema kuwa uwiano wa wafanyakazi wazalendo na wageni katika miradi ya madini na uchimbaji wa mafuta itapangwa na mwekeaji mwenyewe kulingana na kazi zilizopo.

Monday, December 10, 2007

SUALA LA MADINI; Tatizo ni Sheria au Uwezo wa TRA?

RIPOTI ya Kamati ya kupitia mikataba ya madini iliyoongozwa na aliyepata kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Lawrence Masha, imeanika udhaifu wa kitengo cha madini katika wizara hiyo pamoja na Mamlaka ya Mapato nchini katika kusimamia na kuratibu sekta ya madini nchini.

Ripoti ya Kamati ya Masha inasema ushahidi uliotolewa na Alex Stewart (Assayers) Government Corporation unaonyesha dhahiri kuwa uwezo wa TRA kuwa ni mdogo katika masuala ya madini kwa kuwa haina wafanyakazi wa kutosha na wenye ujuzi mpana wa kunyambulisha taarifa za fedha za makampuni ya madini.

Aidha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ambayo Tanzania imenasa nakala yake, suala la udhaifu wa Kitengo cha Madini katika wazara, lilishabainishwa katika ripoti ya kamati ya Dk Kipokola.

Kamati ya Dk Kipokola ilianisha udhaifu wa kitengo hicho katika masuala ya muundo wake, uwezo pamoja uratibu na mawasilaino na idara nyingine za serikali.

“Ripoti )ya Dk Kipokola) inabainisha kuwa muundo wa kitengo cha madini uliopitishwa mwaka 2001 hauendani na matakwa ya sekta hii ambayo inakuwa kwa kasi,” inasema sehemu ya ripoti ya Kamati ya Masha, ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ripoti hiyo inarejea uzoefu ulioonekana katika nchi za Botswana na Ghana na kueleza mathani kuwa nchini Botswana, kuna kitengo cha uchumi wa madini, ambacho jukumu lakwe kubwa ni kulinda maslahi ya nchi kwa kuratibu kwa karibu shughuli za uchimbaji madini.

Nchini Ghana, kipo kitengo ambacho kazi yake kubwa ni kufuatilia kwa karibu gharama za miradi mikubwa ya uchimbaji madini, inasema ripoti hiyo.

Kutokana na masomo hayo, tayari mapanedekezo yalishafikishwa serikalini kuhusiana na umuhimu wa kukifanyia kitengo hicho mabadiliko, lakini kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Masaha, utekelezaji wa mapendekezo hayo unategemea sana mafunzo kutoka Botswana.

Kuhusu TRA, ripoti hiyo inasema kuwa ripoti iliytoandaliwa na Alex Stewart (Assayers) Government Corporation, mannuzi kutoka nje yaliyofanywa na makampuni ya madini hayakuchunguzwa ipasavyo na Idara ya Ushuru wa Forodha kuhusu idadi, aina na thamani ya vifaa vilivyoagizwa ambavyo vinastahili kusamehewa ushuru.

Inabainishwa pia katika ripoti hiyo kuwa ukaguzi wa kina katika maeneo ya amchimbo ulifanyika mara chache sana kabla masuala ya makampuni ya madini hayajahamishwa kutoka idaya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Mapato na kupelekwa Idara ya Walipoa Kodi Wakubwa.

“Kodi zilikadiriwa kutokana na ukagusi uliofanyika ofisini tu. Ziara ya maeneo ya machimbo zilifanywa kwa ajili ya marejesho ya VAT na kodi ya zuio,” inabainisha ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema kuwa Alex Stewart ilibaini kuwepo kwa uwezo mdogo katika ngazi mbalimbali ndani ya TRA kuratibu shughuli za kampuni za kuchimba madini.

“Kwanza TRA ilitakiwa iwe na udadisi wa hali ya juu kuhusu biashara na taarifa za fedha zinazowasilishwa na kampuni za madini… kuna uwezekano kuwa TRA haina watu wenye maarifa maalum kunyambulisha shughuli za kampuni za madini,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa kuna masuala ambayo TRA ilitakiwa iyabaini mapema kama vile muendelezo wa kukosekana kwa nyaraka kadhaa.

“Kuna ushahidi wa dhahiri wa dhamira ya ku[potosha pale madau wawili katika mradi wanapotoa taarifa mbili tofauti za fedha kuhusiana na shehena moja ya dhahabu iliyosafirishwa nje,” inasma ripoti hiyo.

Ikiweka wazi, ripoti inataja tukio ambalo kampuni mbili zilizoungana katika mradi mmoja wa madini, zilidanganya kuhusu mapato ya mauzo ya dhahabu kwa pungufu ya dola za Marekani 2,340,000 kati ya 2001 na 2003.

Monday, December 3, 2007

Niliyoyakuta Addis Ababa

WAKATI Tanzania ilipoamua kuachana na sera za siasa ya ujamaa (na kujitegemea?), zilitolewa sababu zilizolenga kutuaminisha kuwa mfumo huo ulikuwa umefeli kuijenga nchi na kuipeleka katika mstari tulioutaka.

Lakini nchi nyingine ya Kiafrika, Ethiopia, inaonyesha uzoefu tofauti, kwamba ujamaa, iwapo utatekelezwa ipasavyo, bado una nafasi ya kuijenga nchi.

Ingawa maisha ya Waethiopia si tofauti sana na watu wengine wa bara la Afrika, lakini kung’ang’ania kwake sera za ujamaa, kwa kiasi fulani kumewasaidia baadhi ya wananchi ambao ni maskini na wale wa daraja la kati.

Kama unaingia kwa ndege, unapowasili Uwanja wa Ndege wa Dole tu, unaanza kuona tofauti iliyopo kati ya Ethiopia na nchi nyingi za Kiafrika.

Uwanja wake ni mkubwa na unapendeza sana kwa jengo lake kuwa lenye madirisha makubwa ya vioo, ingawa hauna pilika sana sana. Labda haukuwa na pilika kwa sababu tulifika usiku, na safari nyingi zilikuwa zimeshafanyika.

Kitu kimoja ambacho kitakushangaza, kama umetokea mahali ambako muda unathaminiwa sana, ni ufanyaji kazi wa taratibu wa wafanyakazi hawa wa uwanja wa ndege wa Dole.

Nilipata uzoefu huo mara baada ya kutua kwani ilichukua muda wa zaidi ya saa moja kupata visa ambayo maombi yake tayari yalishafanywa wiki kadhaa zilizopita.

Taarifa kuhusu maombi hayo ya visa zilikuwepo katika mafaili machache ambayo yalikuwepo katika meza za watoa visa wapatao watano niliowakuta baada ya kuteremka kwenye ndege.

Lakini cha kustaajabisha ni kuwa mfanyakazi wa kwanza alichukua faili moja na kutazama makaratasi yote hadi mwisho na kunifahamisha kuwa jina langu, pamoja na mwandishi mwenzangu ambaye nilikuwa naye pamoja, hayakuwemo katika faili hilo.

Alituelekeza kwa ofisa wa pili ambaye alikuwa na hati kadhaa za kusafiria ambazo alikuwa anazishughulikia. Tulimsubiri na alipomaliza alichukua hati zetu na kurudi tena kwenye lile faili.

Alilipitia taratibu, lakini hadi mwisho hakufanikiwa kuyaoona majina yetu. Walianza kutuuliza iwapo tuna barua za mwaliko wa mkutano ambao tulikuwa tumekwenda kuhudhuria.

Niliwajibu kuwa sikuwa na barua hiyo katika karatasi, lakini ipo kwenye kompyuta yangu ya mkononi, hawakuonyesha kuwa na nia ya kutaka kuiona hata humo kwenye kompyuta na wakawa wakijibishana wenyewe kwa lugha yao ambayo sisi hatukuielewa.

Inaelekea hawakupata suluhu kwani walirejea tena kwetu na kutuuliza tena kuhusu taasisi ambayo ilikuwa imetualika.

Hii ilikuwa baada ya kufuatilia jina la taasisi kwa zaidi ya mara kumi na wao kuangalia faili lao zaidi ya mara nne.

Nikaamua kufungua kompyuta yangu na kufungua barua ya mwaliko, nikawaonyesha. Mmoja wao akaisoma alipofika katikati akaacha kuisoma akaitisha tena faili na kuanza kupitia upya.

Hakufanikiwa kuona majina yetu. Baada ya kushughulikia watu wengine kadhaa, ofisa yule wa mwanzo alilichukua tena lile faili na safari hii akawa analipitia jirani na aliposimama mwenzangu ambaye nilikuwa nimefuatana naye akiwa umbali wa mita moja na nusu.
Alipopekua ukurasa kama wa nne, aliupitia taratibu na wakati anataka kufungua ukurasa wa tano, yule mwenzangu akamuonyesha majina yetu ambayo alikuwa ameshayapita. Tulishangaa sana iweje wayapite majina hayo kwa zaidi ya mara saba walipoliangalia faili, lakini tukaweza kuyaona, tena kwa mbali!

Hapo ndipo tukapatiwa visa. Shughuli za uhamiaji zilichukua zaidi ya dakika 15 ingawa tulipofika kwenye mstari sisi ndio tulikuwa wageni pekee tunaohitaji huduma hiyo.

Spidi yao kwa kweli inakatisha tamaa na hadi wakati tunafanikiwa kutoka nje ya uwanja, dereva aliyekuwa ametumwa kutufuata alikuwa amesubiri na kukata tamaa kuwa hatukuwepo katika ndege hiyo na akaamua kuondoka. Ilitupasa kukodi teksi hadi hotelini.

Nilianza kupata wasiwasi kuhusu nchi hii ambayo hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika. Lakini wasiwasi huo uliondoka na kuingiwa na mshangao wakati ‘shanta’ alipokuwa anatupeleka kwenye teksi.

Nilipokuwa katika ndege nilipitia jarida ambalo moja kati ya taarifa zilizokuwepo ni kwa mgeni kuhakikisha kuwa iwapo unakodi teksi za watu binafsi, ambazo zina rangi za bluu, ni kupatana bei kwanza kwani hazina bei maalum.

Hivyo tulipoamua kukodi teksi, kitu cha kwanza nilichokifanya ni kupatana bei na wakati tunapatana, kwanza ‘shanta’ alitaka kujua iwapo tutamlipa kwa dola za Marekani au kwa Birr, ambayo ni fedha za Ethiopia.

Nilipomueleza kuwa sikuwa na fedha za nchi yao, aliniambia kuwa itakuwa ni dola 10. Nikamuuliza kama ningekuwa na fedha zao ingekuwa kiasi gani kwa safari hiyo, akaniambia ingekuwa Birr 90 kwani dola moja hubadilishwa kwa Birr tisa.

Hapo ndipo nilipoanza kushangaa jinsi fedha ya nchi hii ilivyo na nguvu! Tulipoingia kwenye taxi na kutoka uwanja wa ndege, dereva alituomba radhi kuwa anapaswa kuongeza mafuta, akaingia katika kituo cha mafuta. Yaani kama madereva teksi wa Dar es Salaam!
Nilipatwa na mshangao zaidi nilipogundua kuwa kwa bei niliyoizoea Dar esSalaam, lita moja ya petroli inauzwa kwa zaidi ya dola moja, jijini Addis Ababa bei ya lita ya petroli ilikuwa haijafikia hata nusu dola.

Lita moja ya petroli inauzwa Birr 7.7, ambayo ni chini kabisa ya dola moja ya Marekani wakati nilitarajia kuwa bei ya mafuta hapa ingekuwa kubwa sana kwa sababu Ethiopia inapata mafuta yake yote kupitia barabara kwa sababu haijapakana na bahari.

Lakini unapoingia mitaani, unakutana na ombaomba kama ilivyo Dar es Salaam, inaonekana wana mitaa yao maalum kwa ajili ya kazi hiyo.

Na wapo wengi sana ingawa kuna mgawanyiko wa tabaka hilo unaoonyesha kuwa ni watu wa jamii fulani tu ambao wengi wao ni ombaomba.

Nilipokutana na Mengesha Melekot, ambaye ni raia wa Ethiopia anayefanya kazi katika taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung (FES) katika ofisi ya Addis Ababa, ambaye ana uelewa mkubwa kuhusu masuala ya uchumi na siasa za nchi hii, alinifahamisha kuwa pamoja na kuwa Ethiopia haina vitu vingi sana vya kuuza nje, lakini kwa miaka mingi limebakia kuwa ni taifa ambalo lilijitosheleza na mahitaji yake kutokana na vitu vinavyozalishwa ndani.

“Hapa hatuagizi vitu vingi kutoka nje. Watu wengi wanakula chakula wanacholima wenyewe, wanajifumia nguo zao wenyewe… hawahitaji nguo kutoka nje, wengi hawategemei vitu kutoka nje,” alisema.

Melekot aliniambia kuwa ni asilimia kumi tu ya mahitaji yanaagizwa kutoka nje na hii inahusisha vitu ambavyo vinatakiwa sana maeneo ya mijini.

Akizungumzia bei ya mafuta, alisema serikali bado inafuata sera za kijamaa na inadhibiti bei ya mafuta. Licha ya kudhibiti, serikali pia inatoa ruzuku kwa bidhaa hiyo muhimu katika uchumi wa nchi na maisha ya watu ili kuhakikisha kuwa inawalinda wananchi wake.

“Pia serikali inadhibiti baadhi ya bei ya vitu, hasa vile muhimu katika maisha ya binadamu. Hii inasaidia kuhakikisha kuwa watu hawapati matatizo makubwa kutoka kwa wafanyabishara ambao mara zote lengo lao ni kupata faida kubwa,” alisema na kuongeza kuwa serikali bado haina nia ya kubadili mfumo wa uchumi wa nchi hiyo.

Ethiopia ni nchi pekee barani Afrika ambayo haikutawaliwa. Ni nchi pekee ambayo ina alfabeti zake na imeshikilia lugha yake ya asili kama lugha ya taifa. Ni nchi ambayo ina kituo kimoja tu cha televisheni, kinachomilikiwa na serikali.

Katika wiki moja niliyokuwapo hapa, sikupata kuona muziki wa magharibi ukipigwa kupitia kituo hiki. Hata kusikia matangazo kwa lugha nyingine tofauti na Hamharik, ambayo ndiyo lugha ya taifa.

Ni nchi pekee ya Kiafrika ambayo ambayo historia yake imefikia milenia mbili. Ni nchi ambayo licha ya matatizo makubwa ya ukame yaliyoifanya dunia iamke, bado uchumi wake unakwenda vizuri licha ya kuwa ina wananchi wengi ambao ni masikini.

Lakini hali hii inabadilika kwa kasi kutokana na utandawazi. Maingiliano na nchi nyingine yanabadilisha mambo Ethiopia kwa kasi.

Na madhara ya mchanganyiko huu unaotokana na utandawazi yanaanza kuonekana wazi miongoni mwa wananchi wa Ethiopia.

Leo hii si ajabu kukuta ghorofa la kisasa lililojengwa kati ya vibanda vilivyojengwa kwa makaratasi ya plastiki katika Jiji la Addis Ababa. Wakati wanaofanya kazi katika majengo hayo ya kisasa wakifika kazini hapo kwa magari yao ya kifahari, watu kutoka katika mabanda hayo, hushinda kando ya barabara karibu na jengo hilo wakiomba chochote kutoka kwa wapita njia.

Mbaya zaidi, wale wanaofanya kazi ndani ya jengo hilo wanawaona hawa kama wanaowaharibia mandhari ya jengo lao wakati wao ndio waliwavamia, wakajipatia ardhi kati yao na kuonyesha utajiri wao bila kukumbuka kuwasaidia wenyeji waliowakuta hapo.

Tayari kampuni kubwa za kigeni zimeshaanza kuingia kwa uwekezaji nchini humu na wananchi wanaanza kuona tofauti ya maisha kwani wageni hawa wanakuja na athari nyingi za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Saturday, December 1, 2007



Lakini hakuna kizuri kisichokosa kasoro. Huu ni mchanganyiko wa aina yake wa majengo katikati ya jiji la Addis Ababa. Kama unavyoona, jengo la ghorofa kadhaa, ambalo ujenzi wake ni wa thamani kubwa, likiwa limezungukwa na vibanda vya wenzangu na mimi, ambavyo baadhi vimeezekwa kwa makaratasi ya plastiki. Ni utajiri katikati ya umaskini na haya ndiyo aina ya maisha ambayo waafrika wengi tunalazimishwa kuyaishi na viongozi wetu. Picha hii niliipiga siku chache zilizopita nilipokuwa Addis Ababa. Hili ni eneo ambalo lipo meta kama 50 tu kutoka yalipo makao makuu ya Umoja wa Afrika
Huu ni mchoro wa kisanii wa Jengo jipya la Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU), ambalo wachina wamekubali kulijenga jijini Addis Ababa. Wachina walitoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa China/Afrika (SinoAfrika) uliopita, kama zawadi yao kwa AU. Kwa kuitikia wito huo, na labda kwa kutaka makao makuu hayo yaendelee kuwa nchini mwao, Ethiopia imetoa eneo kubwa tu, ambalo lipo kando ya makao makuu ya sasa, kwa ajili ya ujenzi huo.
Niliipata picha hii hivi karibuni nilipozuru Makao Makuu ya AU.