Friday, April 25, 2008

Mkapa achunguzwa

SERIKALI imesema kuwa imeshaanza kufuatilia taarifa za tuhuma kuhusu matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya viongozi wa serikali ya awamu ya tatu na iwapo itathibitika walitenda makosa watawachukuliwa hatua zinazostahili.

Kauli hiyo ilitolewa Bungeni jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), aliyetaka kujua serikali inawashughulikia vipi viongozi wa serikali ya awamu ya tatu, wakiongozwa na rais smataafu Benjamin Mkapa, wanaodaiwa kutumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kueleza kuwa inawachunguza watendaji wake wa serikali iliyopita na ni hatua tofauti na kauli iliyowahi kutolewa na rais Jakaya Kikwete, akitaka watu ‘wanaomfuatafuata’ rais Benjamin Mkapa wamwache apumzike.

Katika swali hilo la moja kwa moja, Hamad alisema baadhi ya viongozi chini ya rais Mkapa, walianzisha kampuni binafsi ilhali sheria ya maadili ya umma ya mwaka 1995 hairuhusu kiongozi kuitumia ofisi ya umma kwa maslahi binafsi au biashara.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema serikali inazifuatilia taarifa hizo na kama ikijiridhisha na ukweli wa taarifa hizo, itachukua uamuzi ambao utakuwa na maslahi kwa taifa.

“Ni kweli hivi karibuni kumeibuka kwa tarifa hizo za viongozi kutumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi, lakini kwa upande wetu ni lazima tujiridhishe, ili tutakapoamua tuamue kwa maslahi ya taifa,” alisema Pinda.

Aidha, katika swali la nyongeza, Hamad alitaka kujua ni kwa nini serikali inatumia muda mrefu kutoa uamuzi wa jambo hilo, wakati Wakala wa Usali wa Biashara na Makampuni (BRELA) wanazo taarifa za viongozi hao kufungua kampuni ya kibiashara.

Aidha, alihoji ni kwa nini wahalifu wengine wanafikishwa mahakamani haraka na hukumu zao kutolewa, lakini kwa viongozi hao mambo yao yanachelewa.

“Mimi sioni ni kwa nini serikali haitoi uamuzi mara moja wakati jambo liko wazi na hata BRELA wana taarifa za viongozi hao, na kwa nini hawapelekwi mahakamani?” alihoji Hamad.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni lazima watu watofautishe sheria ya maadili ya viongozi wa umma na sheria ya makosa ya jinai.

Alisema ni vigumu kuwapeleka viongozi hao mahakamani kwani bado hawajawa na ushahidi wa kutosha kujua kama kosa lilofanywa ni la jinai au la maadili ya umma.

Alisema makosa ya maadili ya umma ni lazima kwanza wayaangalie kisiasa na kama yatathibitika kuwa ni ya jinai ndipo humpeleka mtu mahakamani.

“Suala la kumpeleka mtu mahakamani ni jambo kubwa sana na kabla ya kufanya hivyo ni lazima ujue kosa alilofanya ni la jinai au la kukiuka maadili ya umma, lakini kama tutajiridhisha na kile kilichofanyika ni jinai basi tutapeleka kunakohusika,” alisema Pinda.

Majibu hayo ya Serikali ni yametafsiriwa na baadhi ya wabunge kuwa ni ishara ya kuelekea kuchukuliwa hatua dhidi ya viongozi wa serikali ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi.

Miongoni mwa mambo ambayo Mkapa na aliyekuwa Waziri wake Daniel Yona, wanahusishwa nayo ni kumiliki kampuni ya kuzalisha umeme ya Tanpower Resources Ltd.

Kampuni hiyo inahusishwa na mkataba wa kujiuzia mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya kwa bei ya kutupa ya sh milioni 700 na katika mazingira yanayozua maswali mengi hadi hivi sasa, walilipa sh milioni 70 tu na kukabidhiwa mradi huo ambao inaelezwa kuwa thamani yake inazidi sh bilioni 4.

Aidha, kampuni hiyo iliingia mkataba wa kuiuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao itakuwa ikijipatia sh milioni 146 kila siku.

Hii ni mara ya pili kwa tuhuma dhidi ya Rais Mkapa na viongozi wake kutajwa bungeni baada ya juzi Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), kuwatuhumu viongozi hao kumiliki kampuni ya uzalishaji umeme kinyume na taratibu za maadili ya umma.

Aidha, mbunge huyo alisema huo ni mfano mbaya zaidi kwa taifa hasa kwa mawaziri vijana wanaopewa nafasi ya kuziongoza Wizara nyeti.

Wednesday, April 23, 2008

HALI TETE UDSM

SERIKALI imetangaza kuwafutia udahili wanafunzi takribani 300 wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kutokana na vurugu zilizodumu kwa muda sasa chuoni hapo.

Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa Bungeni na waziri wa Elimu na Mafunzio ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, ambaye alisema wanafunzi hao wamafukuzwa kutokana na kukiuka amri ya uongozi wa chuo hicho.

Akiwasilisha tamko la kuwafutia udahili wanafunzi hao jana jioni, Profesa Maghembe alisema kuwa miongoni mwa waliofutiwa udahili ni wanafunzi 39 ambao walikamatwa na Polisi katika vurugu ziliztokea chuoni hapo juzi.

Miongoni mwao, 38 jana walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi tatu tofauti.

Profesa Maghembe alisema kuwa pamoja na hao 39, pia wanafunzi wengine zaidi ya 250, ambao waliandamana juzi na jana na kugoma kuingia madarasani, nao wamefutiwa udahili.

Alisema kuwa inasikitisha kuwa wanafunzi hao walikaidi agizo lililotolewa na uongozi wa chuo kuwataka warejee madarasani na serikali haiwezi kuivumilia hali hiyo.

Wakati huo huo, wanafuzni 38 waliokamatwa juzi kutokana na vurugu hizo, jana walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya vurugu chuoni hapo, kumjeruhi askari na mwenzao mmoja.

Wanafunzi hao ambao wamefunguliwa mashitaka matatu tofauti, walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya mahakimu watatu tofauti.

Mwendesha Mashitaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela, aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Mohamed Rashid (24), Blessas Lyimo (21), Mtaha Frank (24), Natanael Innocent (22), Kisendi Rashid (24), Rahel Chasaba (22), Ester Sanga (21), Lutandilo Hosea (22), Mgaya Risper (24) na Rose Casmir (21).

Wengine ni Lugome Claus Daud (25), Mbaraka Charles (23), Abdallah Selemani (23), Charles Peter (24), Kizito Prim (23), Deodatus Ngoti (28), Juma Athumani (25), Gabriel Gibson (23), Chogelo Gregory (22) na Mwankunga Edgar (25).

Wanafunzi wengine wametajwa kuwa ni Munish Hilary (22), Patrick Yesaya (22), Alex Manonga (22), Maliwa Nyasilu (22), Abrahamani Ephraimu (23), Bugumia Matiko (22), Mtandika Miraji Andrew (27) na Maige Emmanuel (24).

Wengine ni Masudi Salehe (20), Mdeme Ramadhan (23), Jalud Said (23), Lutaiwa Frenk (22), mwasyeba Anosisya (24), Shahamila Royald (23), Ahmad Masasi (22), Fimbo Yoseph Frednand (25), Halima Mfaume (23) na Stella Kambanga (24).

Katika kesi ya kwanza ambayo inawahusisha wanafunzi wote 38, Kamishna huyo Msaidizi wa Polisi alidai mbele ya Hakimu Hassan Makube kuwa juzi, muda usiofahamu katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanafunzi hao walikula njama ya kuwafanyia fujo wanafunzi wenzao na wahadhiri, kwa lengo la kusababisha uvunjifu wa amani.

Alidai siku hiyo hiyo majira ya saa 10:50 jioni katika eneo hilo la chuo walifanya vurugu kwa kuwazuia wanafunzi na wahadhiri kuingia madarasani na kuwachapa, hali iliyosababisha uvunjifu wa amani.

Katika kesi nyingine iliyopo mbele ya Hakimu Saidi Msuya, wanafunzi 13 kati ya hao wanadaiwa kuwa juzi, muda usiofahamia eneo la chuo hicho, waliwajeruhi wanafunzi waliokataa kuungana nao kufanya vurugu chuoni hapo.

Mwendesha Mashitaka alidai siku hiyo hiyo, washitakiwa na waliimjeruhi mwanafunzi mwenzao, Rashid Ally kwa kutumia fimbo na mawe na kumsababishia maumivu.

Katika kesi ya tatu iliyopo mbele ya Hakimu Euphemia Mingi, wanafunzi 11 wanadaiwa kumjeruhi Ofisa wa Polisi aliyekuwa kazini.

Mwendesha Mashitaka, alidai katika tukio hilo lilitokea juzi, saa 7.30 mchana, wanafunzi hao walimjeruhi Polisi mwenye namba E 8464 Konstebo Petro, aliyekuwa kazini na kumkata kwa chupa katika mguu wa kulia.

Washitakiwa wote hao walikana tuhuma hizo na baadhi yao kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti. Masharti hayo ni kuwa na dhamini wawili wa kuaminika. Kesi hizo zitatajwa Mei 6 mwaka huu.

Wakati hayo yakitokea, hali ya mgomo iliendelea jana katika maeneo ya UDSM, ingawa hakukuwa na vurugu kama juzi.

Hata hivyo, akizungumza chuoni hapo, Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Rwekaza Mkundala, aliwakana wanafunzi waliogoma na kusema kuwa si wanafunzi wake.

Jana kutwa nzima wanafunzi hao walikusanyika nuje ya majengo ya utawala, huku askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa wameweka kambi chuoni hapo wakiwa na zana zao tayari kwa lolote litakalotokea.

Pamoja na madai ya kutaka wenzao takribani 20 waliosimamishwa warejeshwe, jana waliongeza dai jingine, wakitaka wenzai 38 waliokamatwa juzi wakati wa vurugu, waachiwe.

Hali ilizidi kuwa ya wasiwasi baada Askari wa Kikosi cha FFU kurejea tena chuoni hapo wakiwa kwenye magari zaidi ya nane likiwemo moja la kurusha maji, ingawa hawakupambana na wanafunzi kama juzi.

Hadi jana jioni hapakuwepo dalili za maelewano ya kusitisha mgomo huo, huku habari zikienenezwa na wanafunzi kuwa kuna mwanafunzi mmoja alifariki dunia baada ya kuzidiwa na moshi wa mabomu.

Akijibu maswali ya waandishi baada ya kikao na ujumbe kutoka Comoro, Profesa Mukandala alikiri kuwa suala la mgomo huo ni kubwa, lakini hafikiri kukifunga chuo haraka bila kupata amri kutoka Serikalini, licha ya wanafunzi kukaidi amri iliyowataka waingie madarasani.

Alisema kuwa wanafunzi wanaogoma ni wale ambao wameshindwa kujilipia ada. Akifafanua, alisema kuwa awali wanafunzi hao walimwendea wakamuomba nafasi ya kujiunga chuo Kikuu kwa maelezo kuwa wataweza kujilipia wenyewe.

Alisema baada ya kufanya mazungumzo na wakuu wa vitivo, zikapatikana nafasi zaidi ya 400 na wanafunzi hao waliruhusiwa kujiunga kwa sharti la kujilipia wenyewe.

Hata hivyo, profesa Mukandala alisema kuwa baada kusoma kwa kipindi cha muhula mmoja, wanfunzi hao waligoma kuendelea kulipa ada na sasa wanashinikiza chuo kifungwe, jambo analopingana nalo.

“Sisi tusingependa kufunga chuo kwani tunafahamu kwani ni usumbufu mkubwa na hasara,” alisema.

Wakati akitoa madai hayo kwa upande mwingine wanafunzi walikuwa wakiandamana katika maeneo ya chuo hicho wakipaza sauti zao wakitaka uongozi wa chuo ujiuzulu na wale wenzao 38 waliokamatwa juzi na Polisi waachiwe, ili waungane kudai wenzao waliofukuzwa.

“Hatuwezi kuingia madarasani kama wanavyotaka hadi wawaachie na kuwarejesha wenzetu waliokamatwa bila hatia na Polisi, ili tusaidiane kuwadi haki,” alisisitiza mmoja wao.

Kelele za mayowe zilizidi kutawala eneo la utawala wa chuo baada kuenezwa taarifa kuwa kuna wanafunzi watatu wamefariki, akiwemo mmoja mjazito aliyeripukiwa na mabomu ya kutoa machozi.

“Dada yetu mpendwa wetu ameuawa bila hatia na wanafunzi wenzetu wamekamatwa bila kufanya ghasia… Mukandala damu isiyo na hatia inakulilia… jiuzulu,” lilisema bango moja lililobebwa na mwandamanaji.

Hata hivyo, madai ya kufariki kwa wanafunzi yalikanushwa na uongozi wa chuo kwa maelezo kuwa wanafunzi wanne na wafanyakazi wawili ndio walipata majeraha kidogo wakati wanakimbia na wote wametibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Alisema anayedaiwa kufariki, Neema Hamidu, yu hai lakini amepelekwa kwenye zahanati moja huko Mikocheni kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya kushtuka kutokana kuwa na ujauzito.

Mwanafunzi huyo anakaa katika Hostel za Mabibo.

Pia Profesa Mukandala alikanusha tuhuma alizokuwa anaelekezewa kuwa yeye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ndugu zangu hata nafasi hii mimi sikuiomba, niliitwa nikafanyiwa usaili nikaonekana nafaa, wala sijawahi kuhudhuria mkutano wa CCM Butiama,” alisema Profesa Mukandala huku akisisitiza kuwa anaongoza chuo kwa kufuata kanuni na taratibu za chuo.

Licha ya wanafunzi hao kuendelea kusisitiza kuwa wataingia darasani ikiwa tu wenzao watarejeshwa, uongozi wa chuo hicho ulishikilia msimamo wao kuwa wanafunzi 14 kati ya 20 hawatareshwa chuoni na sita walianza kuhojiwa jana, akiwemo Waziri Mkuu wa serikali ya wanafunzi, Julis Mtatiro.

Kwa upande mwingine, migogoro inayoendelea sasa inadaiwa kuibuliwa na hatua ya uongozi kufuta uchaguzi wa rais wa Daruso kwa madaai kuwa hizo ni njama za kutaka mgombea anayeungwa mkono ya uongozi wa chuo ndiye ashinde.

Wakati hali hiyo ikitokea, mgombea mmoja, ambaye ni raia wa Uganda, Odong’ Odwar, alizuiwa kuwania nafasi hioyo kwa madai kuwa hajawasilisha vyetu vyake vya elimu. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika kesho na jina la mgombea huyo halimo miongoni mwa wagombea.

Baada ya uchaguzi huo kumamishwa wanafunzi watano waliokuwa karibu na mgombea huyo walifukuzwa chuo kwa madai kuwa walikuwa wanavunja taratibu za chuo, ili kumvunja nguvu Odwar na baadaye alisimamishwa masomo kwa maelezo kuwa, kuna angalizo lilitolewa kwa utawala kuhakiki uhalali wake wa kuwepo chuoni hapo, pamoja na kupeleka nyaraka za matokeo (result slip)

Licha ya kupeleka nyaraka hizo uongozi huo ulidai cheti halisi na baada ya hilo kutokea, Odwar aliomba kwa baraza la mtihani la Uganda kuandika barua inayoeleza kuwa bado vyeti hivyo havijatolewa, jambo ambalo uongozi wa UDSM umelikataa.

Pia wanafunzi hao wanadai baada ya utawala kusimamisha uchaguzi huo, ili azma yao itimie waliamua kuwashawishi wajumbe wa bodi ya Rufaa ya Uchaguzi kujiuzulu ili kiwe kama kisingizio cha kuendelea kukwamisha uchaguzi huo na baada ya kugundua kuwa Waziri Mkuu wa Daruso, Julias Mtatiro ana mpango wa kutumia Bunge la chuo kuhoji walimsimamisha kusimamishwa kwa uchaguzi huo.

Tuesday, April 22, 2008

Chenge na siri yake ya vijisent

Aliyewahi kuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, aliyejiuzulu Jumapili iliyopita, sasa amewaomba waandishi wa habari wamwache ili kumpatia muda wa kutafakari matatizoyanayomkabili.
Chenge anasema kuwa matatizo yanayomkabili ni makubwa na angependa kupata muda wa kuyatafakari bila bughudha. Alisema kuwa kwa sasa hana mpango wa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa Chenge amepanga kutoa taarifa ndefu ya kufafanua jinsi ambavyo fedha kiasi cha dola milioni moja zilivyoingia kwenye akaunti yakeiliyopo katika benki moja huko katika kisiwa cha Jersey, Uingereza.
Lakini kauli hiyo inaweza kumtia Chenge au mtu au watu wengine katika matatizo zaidi kutokana na uchunguzi unaofanywa na Serious Fraud Ofice (SFO) ya Uingereza kwani anawezakutoa taarifa ambazo wachunguzi hao hawana na wakaanza kuzifuatilia na kuibua mambo mengine mengi.

Ditopile azikwa Dar

Rais Jakaya Kikwete ameongoza mazishi ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Ukiwaona Ramadhan Mwinshehe Ditopile Mzuzuri, aliyefariki Jumapili iliyopita katika hoteli ya Hikux mjini Morogorogo.
Mazishi hayo yamefanyika leo katika shamba la marehemu huko Kinyerezi,nje kidogo ya Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wengine maarufu akiwemo Waziri Mkuu, Mizengi Pinga na mtangulizi wake aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Mazishi hayoyalifanyika saa 10jioni bada ya maiti hiyo kuswaliwa katika msikiti wa Tambaza na salamu za rambirambi kutolewa nyumbani kwa marehemu, Upanga.

Monday, April 21, 2008

Andrew Chenge ajiuzulu

(Habari hii ni kwa hisani ya Tanzania Daima)

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, amejiuzulu wadhifa huo kuanzia jana kwa kile alichoeleza kuwa ni kulinda masilahi ya taifa.
Chenge, ambaye anakabiliwa na tuhuma za kumiliki zaidi ya dola milioni moja za Marekani katika akaunti yake iliyopo Kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza, jana alimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kuomba kujiuzulu, ambayo rais aliiridhia.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima jana usiku, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alithibitisha rais kupokea barua ya Chenge ya kuomba kujiuzulu wadhifa wake.
Alisema rais aliridhia barua hiyo, huku akimkariri akisema kuwa kwa mazingira ya wakati huu uamuzi huo unafaa kuchukuliwa.
Aidha, mkurugenzi huyo akikariri barua ya Chenge, alisema amefikia uamuzi huo ili kulinda masilahi ya nchi pamoja na kwamba uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Chenge umefikiwa baada ya mashauriano kati yake na Rais Kikwete.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa kufikiwa kwa uamuzi huo hakumaanishi kukiri tuhuma hizo, bali kutambua uzito wa tuhuma zinazomkabili.
Aidha, habari zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Chenge umechangiwa na dhamira yake ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuzungumzia kwa kina tuhuma hizo.
Wiki iliyopita, gazeti la The Guardian la nchini Uingereza liliandika kuwa, katika uchunguzi wa SFO iligundulika akaunti moja inayohusishwa na Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni moja iliyopo kwenye Kisiwa cha Jersey.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO inamchukulia Chenge kuwa mtu anayeweza kuwa shahidi muhimu katika uchunguzi wa zabuni ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE System ya nchini Uingereza.
Gazeti hilo liliandika kwamba, SFO inatarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo, ili kuangalia iwapo zina uhusiano na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28 ambazo ni sawa na sh bilioni 70, mwaka 2002.
Hata hivyo, inaaminika kwamba uchunguzi wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo ingawa ule wa awali ulionyesha kuwa moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha zinazoaminika kuwa za Chenge zina uhusiano na zile zilizotoka katika Kampuni ya BAE inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada mbovu kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.
The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, linaripoti kuwa, taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.
Gazeti hilo lilimkariri Waziri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumzia kwa mara ya kwanza tuhuma hizo Jumatano iliyopita, Chenge aliwataka Watanzania kusubiri uchunguzi dhidi yake unaofanywa na SFO.
“Tusubiri uchunguzi ukamilike... kama uthabiti ukithibitisha hata hivyo vijisenti, ijajulikana vilipatikanaje,” alisema Chenge nje ya chumba cha wageni mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akitokea nchini China.
Kutokana na kauli yake ya kuziita mabilioni ni vijisenti, wananchi walionyesha kukerwa na kauli hiyo kwa maelezo kuwa ni dharau, na kwamba huenda atakuwa akimiliki fedha zaidi ya hizo.
Pamoja na hayo, baadhi ya vijana wanaotoka katika vyama kadhaa vya upinzani mjini Dodoma walitangaza azima yao ya kuandamana, ili kumzuia asiingie bungeni wiki hii.
Kutokana na hali hiyo, Chenge alilazimika kuwaombva radhi Watanzania ambao walikwazika au kuumizwa na kauli hiyo.
Chenge alisema halikuwa lengo lake kuwakera wananchi kwa kauli hiyo iliyozua mjadala kiasi cha baadhi ya makundi ya watu wa kada tofauti kutoa maoni yao wakimtaka Rais Jakaya Kikwete amwajibishe.
“Mimi si Mzaramo. Hiki ni Kiswahili. Sisi wengine kule Usukumani kusema vijimambo, au vijisenti, vijitoto hivi ni kawaida kwa desturi zetu.
“Ndiyo maana napenda kusema wazi kwamba iwapo kuna Watanzania niliwaumiza kwa kauli ile niliyoitoa kwa nia njema kabisa na wala si kwa lengo la kuwakejeli, naomba radhi kwa hilo,” alisema Chenge.
Chenge ni waziri wa nne kujiuzulu katika kipindi cha miezi miwili baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu kutokana na kutajwa katika kashfa ya mkataba tata wa kuzalisha umeme wa dharura wa Kampuni ya Richmond.
Mawaziri hao isipokuwa Dk. Msabaha ni miongoni mwa orodha ya mafisadi 11 iliyotajwa na kambi ya upinzani, Septemba 15 mwaka jana katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Aidha, Chenge alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa walioandamwa hasa baada ya kurejeshwa tena serikalini, wakati wa mabadiliko ya mawaziri yaliyotokana na kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri, Februari mwaka huu.

Ditopile afariki dunia

(Habari hii ni kwa hsiani ya Tanzania Daima)
ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, amefariki dunia jana asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Meshack Massi, Ditopile alifariki dunia ghafla jana, saa 3 asubuhi akiwa katika Hoteli ya Hilux, iliyopo mjini hapa.
Dk. Massi alisema Ditopile alifariki dunia akiwa katika hoteli hiyo alipokuwa akiangalia televisheni.
Alisema jana asubuhi alipokea ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) kutoka kwa uongozi wa hoteli hiyo ambako Ditopile alikuwa amepanga kuwa hali yake si nzuri na wangehitaji msaada wa daktari.
“Nikaagiza haraka wauguzi kwenda kumpima, baadaye nikaona wanakuja na gari ndogo na tulipompima tukabaini alikuwa amefariki dunia,” alisema Dk. Massi.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwa gari la jeshi lenye namba 1759 JW 04, kwenda jijini Dar es Saalam ambako umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ukisubiri mipango ya mazishi.
Habari zinaeleza kuwa uchunguzi wa mwili huo unatarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Lugalo, kwani chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika.
Mdogo wa marehemu, Selemani Ditopile, akizungumza na Tanzania Daima jana jioni, alisema marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya familia yaliyopo Kinyerezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia kifo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Said Kalembo, alisema juzi Ditopile alimpigia simu akimfahamisha kwamba yupo mkoani Morogoro na kwa kuwa alikuwa amefika usiku walitafuta nyumba ya kulala.
“Kesho yake hatukuonana, lakini alipomaliza shughuli zake alirudi katika hoteli hiyo. Jana baada ya kuamka akiwa na mkewe wakiwa wanaangalia televisheni ghafla alizidiwa na kuomba msaada wa kidaktari.
“Hata hivyo, baadaye alipomuangalia kwenye viganja vya mkono, vilikuwa vyeupe,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Aidha, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye, alisema walipokea simu ya Dk. Massi iliyoeleza kuwa katika chumba cha ICU mkoani hapo kulikuwa na mwili wa Ditopile.
Alisema taarifa kutoka kwa ndugu aliokuwa nao zinaeleza marehemu alikuwa na ndugu zake wawili, akiwemo mdogo wake, Selemani Ditopile na mkewe Tabia.
“Walifika mkoani hapa Aprili 18, saa 6 usiku na kufikia katika hoteli hiyo kwa ajili ya mapumziko, tayari kwa safari kesho yake kwenda kwenye mashamba yake yaliyopo Mgongolwa, wilayani Mvomero,” alisema kamanda huyo wa Polisi.
Alisema siku iliyofuata walikwenda shambani huko ambako walirudi saa 12 jioni na waliporudi waliwatembelea ndugu na jamaa mkoani hapa, kisha wakarejea hotelini hapo kulala na Ditopile alikuwa amelala chumba namba 106, wakiwa na mpango wa kurejea Dar es Salaam jana.
“Alfajiri inadaiwa marehemu huwa na tabia ya kuswali, kwa hiyo baada ya swala yeye na mkewe huyo walikaa kuangalia televisheni, ambapo mkewe alipitiwa usingizi kidogo, alipoamka akajaribu kumwamsha lakini hali yake haikuwa ya kawaida,” alisema.
Alisema baadaye alimjulisha shemeji yake na kuanza kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa ndani na nje ya mkoa sambamba na kuomba msaada katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye aliwasili mjini hapa jana asubuhi, alisema ameguswa na msiba huo kwa kuwa alimfahamu Ditopile kwa muda mrefu na wamekuwa pamoja jeshini na serikalini.
Alisema kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi ni msiba mkubwa, kwa kuwa alikuwa na mchango mkubwa katika chama na alikuwa akirekebisha kasoro mbalimbali za chama.
Ditopile ambaye pia alikuwa mwanasiasa alifunguliwa kesi ya kumuua kwa kumpiga risasi, dereva wa daladala, Hassan Mbonde, katika tukio lililotokea makutano ya Barabara ya Bagamoyo na Kawe, Dar es Salaam. Tukio hilo linadaiwa kutokea jioni ya Novemba 4, mwaka 2006.
Katika kesi hiyo ambayo awali ilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, Ditopile alikuwa akitetewa na Wakili, Nimrod Mkono.
Baada ya kesi hiyo ya kuua bila kukusudia kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, mahakama ilipanga kutajwa kesi hiyo kwa mara ya kwanza Aprili 24, mwaka huu.
Tukio hilo la mauaji linadaiwa kutokea baada ya gari la mwanasiasa huyo kugongwa na daladala, na kisha dereva akakataa kushuka kushuhudia uharibifu alioufanya.
Kutokana na kitendo hicho, Ditopile-Mzuzuri, anadaiwa alichomoa bastola, akawa anagonga gonga dirisha ili dereva ashuke chini, ghafla, risasi ilifyatuka na kumuua papo hapo.
Kutokana na kukabiliwa na kesi hiyo, siku moja kabla ya kufikishwa mahakamani, Novemba 5 mwaka 2006, Dipotile alimwandikia barua Rais Jakaya Kikwete akiomba kujiuzulu wadhifa wa mkuu wa mkoa. Rais Kikwete alikubali ombi hilo Novemba 7.
Katika barua hiyo Rais Kikwete alisema: “Kuomba kwako kujiuzulu wadhifa wako wa mkuu wa mkoa ni uamuzi wa busara na hekima. Unatoa fursa kwa taratibu stahiki za kisheria kufanyika bila ya vizuizi visivyokuwa vya lazima. Ni heshima kwa taifa letu linalozingatia utawala wa sheria.
“Hivyo napenda kukuarifu kuwa nimekubali ombi lako la kujiuzulu wadhifa wa mkuu wa mkoa. Kwa mara nyingine tena pole kwa yote. Usiache kumshukuru na kumuomba Mungu.”
Katika barua yake ya kuomba kujiuzulu, Ditopile alisema tukio hilo lilikuwa linapingana na dhamira na wajibu wa kazi yake ya ukuu wa mkoa.
Baada ya Ditopile kujiuzulu ukuu wa mkoa, mwanasiasa mkongwe, Abeid Mwinyimusa, aliteuliwa kushika wadhifa huo.
Uteuzi huo wa Mwinyimusa ulianza Novemba 28, mwaka 2006, na aliapishwa Desemba 4, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Kwa kuwa Serikali imezidiwa…

Nilikuwepo katika hoteli ya Movenpick wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema alipowaambia wahariri wa habari kuwa mafisadi wa EPA (akimaanisha watu wanaotuhumiwa kuiba fedha za umma kupitia akaunti ya malipo ya madeni ya nje iliyoko Benki Kuu), ni sawa na magaidi ambao wameiteka ndege.

Mwema alitoa mfano huu kutaka kuwaaminisha wahariri hao kwa nini timu ambayo yeye ni mjumbe wake, inayochunguza wizi huo, inashindwa, si tu kuyataja majina ya watuhumiwa ambao tayari wameshaanza kurejesha fedha walizoiba, bali pia kuwachukulia hatua za kisheria wakati huu.

Akitetea hatua zinazochukuliwa na timu hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, na kumhusisha Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Edward Hosea, kama mjumbe wa tatu, Mwema alisema kuwa iwapo timu yake haitokuwa makini, wezi wa fedha za EPA wanaweza kutenda kama magaidi ambao wanaweza kuilipua ndege waliyoiteka ikiwa na mateka wake ndani.

Nikiri kuwa wakati niliposikia kauli hiyo ya Mwema kwa mara ya kwanza pale Movenpick, sikuona mara moja ukubwa wake. Ilikuwa mkapa siku ya pili, nilipoitafakari wka kina ndipo nilipobaini kuwa kuna uwezekano Mwema, labda kwa lengo la kutaka kujikosha kuwa anachokifanya kipo juu ya uwezo wake, aliamua kuonyesha kimafumbo ni jinsi gani mafisadi wameikamata serikali.

Kwa vyovyote vile, katika hali ya kawaida, haiwezekani kwa vyombo vikubwa vilivyokabidhiwa dhamana ya kutunza sheria katika nchi kama vile ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wapate ushahidi dhahiri dhidi ya wezi, halafu washindwe kuwachukulia hatua.

Na hivi ndivyo ilivyotokea kwa uchunguzi unaofanywa na vyombo hivi ndivyo ilivyotokea kwani timu hii baada ya kuwahoji wezi hao, ilipata ushahidi wa dhahiri kiasi kwamba baada ya mashauriano, wezi waliona kuwa hakuna njia nyingine ya kukataa kosa hilo na wakaamua kuanza kurejesha fedha hizo.

Kwamba wamekubali kurejesha ni uthibitisho wa wazi kuwa waliiba, na ndio maana nimeamua bila kumung’unya maneno kwuaita wezi. Kwamba fedha hizo ziliibwa ilishathibitishwa na Ernst & Young katika ukaguzi uliogfanyika na hata rais Jakaya Kikwete alishawishika na kuyakubali matokeo ya uchunguzi huo kiasi cha kufikia uamuzi wa kumfuta kazi aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali.

Katika mazingira ambayo wezi wameamua kurejesha fedha walizoiba, mwendesha mashitaka anahitaaji ushahidi gani mwingine ili kujihakikishia ushindi katika kesi yake? Ni dhahiri kuwa mwendesha mashitaka anapoeleza kuwa haweza hata kuyataja majina ya wezi hao, kuna nguvu za ajabu nyuma ya woga huo.

Kwa kuwa timu hii ilipewa kazi na Rais, ninashawishika kuamini kuwa rais hawezi tena kuwageuka na kuwatisha ili wasifanye kazi yao ipasavyo. Hivyo, ni dhahiri kuwa nguvu hii haitoki katika mamlaka mahsusi zilizopo na hapa ndipo kauli ya Mwema akiwafananisha wezi hawa na magaidi walioteka ndege ilipoanza kunikolea na kupata maana halisi.

Ndio maana sasa ninaamini kuwa serikali imezidiwa na mafisadi katika hili la EPA. Na kwa kuwa serikali imezidiwa na mafisadi, ningependa kuchukua nafasi hii kuwashauri watanzania wenzangu kuwa umefika wakati sasa wa wananchi sisiw a kawaida, kuisaidia serikali katika kupambana na mafisadi. Nashauri tuangalie namna ya kutumia nguvu ya umma ili mafisadi wasiilipue serikali yetu na sisi tukiwa ndani yake, kama ambavyo magaidi wanavyoweza kuilipua ndege na mateka wake.

Awali, kabla hatujalishuhudia hili la EPA, Rais Kikwete alipochagua Baraza jipya la Mawaziri mwezi wa pili, watu wengi waliulalamikia uteuzi wa Andrew Chenge, wakimtuhumu kuwa ni mmoja wa mafisadi. Tuhuma hizi zilimfikia mwenyewe Chenge na alipotakiwa aeleze ni kwa nini, licha ya tuhuma hizo zote, ameteuliwa, yeye aliwaambia wanaohoji hilo waende wakamuulize rais ambaye ndiye aliyemteua.

Mimi nilikuwa ni mmoja wa watu ambao nilimuuliza Chenge hilo na siku ambayo Baraza hilo liliapishwa pale Chamwino, Dodoma. Mara aliponijbu hivyo, nilijaribu kumsogelea rais Kikwete kwa lengo la kulipenyeza swali hilo kutokana na ushauri wa Chenge. Rais alikuwa amezungukwa na watu wengi na alipotuona waandishi tukimnyemelea, alituwahi na kutueleza kuwa asingeweza kusema lolote kwa wakati huo kwa sababu alikuwa ameshasema sana, na kuwa atasema tena siku hiyo jioni kwenye hafla iliyokuwa imeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nilitarajia kuwa rais angelizungumzia hilo katika hotuba yake jioni hiyo, lakini hakuligusia. Labda alikuwa hajui kuwa tulitaka kumuuliza hilo. Lakini siku zilizofuata, bila shaka alisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu tuhuma dhidi ya Chenge na lawama kwake kwa nini aliamua kumteua kuwa waziri. Kwa badati mbaya sana, hadi leo rais hajajibu hilo, licha ya kupata fursa kadhaa za kuzungumza na wananchi.

Sasa kama miujiza vile, habari zinapatikana kuwa kilichokuwa kinadhaniwa kuwa ni tuhuma tu, kinaweza kuwa ni habari ya uhakika; Chenge ni bilionea. Katika hili tatizo si ubilionea wak, bali ameupataje ubilionea huo wakati akiwa mtumishi wa serikali hii ambauyo inanuka umasikini kushoto kulia, mbele nyuma, juu na chini?

Haiyumkini kuwa Rais Kikwete hakuwa na chaguo jingine badala ya Chenge. Nini kimemsukuma kuchagua mtu ambaye uadilifu wake una mashaka, kinaweza kuwa ni nguvu zile zile zilizotajwa na Mwema.

Ninachokihisi hapa ni kuwa kuna uwezekano kuwa rais naye amezidiwa katika hili na ndio maana narejea ushauri wangu kwa watanzania wenzangu kuwa imefika wakati sasa wananchi tujitoe muhanga kumsaidia rais kupambana na nguvu hizi. Naamini kuwa nguvu za umma hazitashindwa.

Uundwaji wa baraza hilo la mawaziri ulitokana nay ale yaliyoibuka baada ya kuwasilishwa bungeni kwa ripoti ya Kamati teule ya Bunge kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa harura uliotolewa kwa kampuni ya Richmond ya Marekani. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasdsa akajiuzulu na Baraza la Mawaziri likavunjika.

Lakini inaonekana kuwa hichio kilikuwa ni kisa tu na sasa mkasa wenyewe unaonekana huko huko bungeni kupitia Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Wakati ripoti hiyo ilipowasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, ilijadiliwa kwa jazba sana. Katika mchango wake wa maandishi, Aziz alituhumu kuwa kamati ilikiuka misingi ya kuundwa kwake kwa kufanya kazi nje ya muda iliyopangiwa, na hivyo kufanikisha kuandaa ripoti mbili, ikiwamo moja ambayo ni bandia (fake).

Hizi ni tuhuma nzito sana na mara moja zilipata mshtuko wa Bunge kama taasisi na kamati kama chombo kilichotekeleza azimio la bunge. Kutokana na hilo, Bunge, kupit6ia tangazo lililotolewa na Spika, Samwel Sitta, lilimtaka Aziz, kuthibitisha kile alichokisema, kama inavyotakiwa katika moja ya kanuni za Bunge zinazokataza Mbunge kusema uongo Bungeni.

Aziz alitakiwa kuthibitisha ukweli ya aliyoyaeleza kwa kuwasilisha maelezo kuhusiana na kauli yake hiyo. Kwa kuwa muda wa mkutano uliojadili masuala hayo ulikuwa umemalizika, Aziz alitakiwa kufanya hivyo katika mkutabno uliofuata.

Lakini tumeshuhudia maajabu kwani Soika huyo huyo, ambaye ndiye aliyetangaza kuwa Aziz anatakiwa kujieleza kwa mujibu wa kanuni, leo hii ameyazuia maelezo ya Mbunge huyo kwa maelezo kuwa kuyawasilisha Bungeni ni kukiuka kanuni kwa sababu kamati inayotuhumiwa ilishamaliza kazi yake kwa hiyo haiwezi kujitetea.

Kinachoshangaza ni kwua wakati uamuazi wa kumtaka Aziz ajieleza ulitolewa na Bunge, uamuazi wa kuyakataa maelezo yake wala haukulihusisha Bunge! Kilikuwa ni kikao cha viongozi wa CCM! Na kwa maneno yake mwenyewe, Aziz amesema kuwa amekubaliana na hoja ya kumzuia kusema Bungeni kutokana na kulinda maslahi ya chama chake.

Haya ni maajabu yaliyoje! Maamuzi ya Bunge yakaamriwe na kikao cha viongozi wa CCM! Hatua hiyo inanilazimisha nijiulize hivi Bunge lina uhusiano gani na CCM kiasi kwamba sehemu ya maamuzi yake yakafanywe na viongozi wa chama hicho? Ndio utaratibu tuliojiwekea huo?

Namshanga pia Spika kwa kusema sasa hivi kuwa Aziz kwuasilisha maelezo yake ni kukiuka kanuni wakati alipoamriwa akalete maelezo zilitumika kanuni hizo hizo. Kwani wakati huo hawakujua kuwa kamati hiyo ilikuwa imemailiza muda wake?

Pia, mapendekezo ya kamati hiyo yalifikishwa serikalini kupitia azimio la Bunge. Serikali ikasema kuwa inakwenda kuyafanyia kazi na itakuja kutoa maelezo yake Bungeni. Hili tunalisubiri. Ninachojiuliza ni kuwa iwapo katika maelezo yake, serikali itaituhumu kamati hiyo kwa jambo lolote, itakuwaje?

Najiuliza swali jingine; hivi itakuwa iwapo mmoja wa wabunge ataamua kuhoji kulikoni, mbona Aziz hajawasilisha maelezo yake kama ilivyokuwa imeagizwa na bunge atyajibiwa nini? Kwamba eti vkikao cha viongozi wa CCM kimeona ni ukiukwaji wa kanuni za bunge kumruhusu alete maelezo yake?

Mlolongo wa maswali haya ambayo kukosekana kwa majibu yake ya uhakika kunazua utata kunaonyesha kuwa si bure, lazima kuna nguvu nyingine ambayo zimesababisha kupindishwa kwa hoja ya Aziz na kuondolewa Bungeni kinyemela hadi kwenye vikao vya viongozi wa CCM ambao walijipa nguvu ya kuamua hoja iliyotolewa Bungeni.

Inaonekana wazi kuwa Bunge limezidiwa na nguvu fulani kiasi kwamba limekubali kupokonywa hoja hii na CCM. Na ndio maana sitachoka kuwaomba watanzania wenzangu kuwa nao wasichoke, tujitolee kulipigania Bunge letu.

Naamini kuwa kwa umoja wetu, tunaweza kuuondoa unyonge tulio nao na kupata nguvu ya kulisaidia Bunge kupambana na nguvu hizi zisizoonekana. Na hapa naomba tuitumie nguvu ya umma kulikomboa Bunge letu.

Kwa ujumla wake, serikali inaonekana kushikwa na kigugumizi tangu tuhuma za ufisadi dhidi ya watumishi wake na wafanyabishara wakubwa, zianze kutajwa hadharani. Tangu wakati huo, serikali haijafanya lolote lililoonekana dhahiri, kuwa ni juhudi zake za kupambana na ufisadi.

Baadhi ya waliokuwa wametajwa katika orodha ya mafisadi na Dk. Wilbrod Slaa, walitishia kwenda mahakamani kwa madai kuwa wamekashifiwa. Hiyo ilikuwa ni hatua nzuri ambayo ingesaidia kuwasafisha lakini kwa mshangao wa wengi, hadi hii leo wameshindwa kufanya hivyo.

Kushindwa kwao ni moja ya dalili kuwa huenda kilichoelezwa na Dk. Slaa ni kweli, na kuwa iwapo mamlaka zinazohusika zingetaka kulishikia bango suala hilo, hapo palikuwa mahali pazuri pa kuanzia. Lakini hadi leo, si jeshi la Polisi, Takukuru wala taasisi nyingine yoyote inayohusika na vita dhidi ya ufisadi ambayo imeonekana kuzifanyia kazi tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa ambazo wahusika wameshindwa kuzikanusha.

Kwa ujumla inaonekana kuwa serikali na taasisi zake zinakwazwa na nguvu fulani ambayo haionekani wazi. Na ndio maana narudia tena kuutaka umma wa watanzania, tujifunge vibwebwe kwa ajili ya kuitetea serikali yetu dhidi ya nguvu hii kubwa ambayo tayari imeshajionyesha dhahiri. Naamini kwua katika umoja wetu tutashinda na kurudisha heshima ya serikali na nchi yetu.

Mungu na atubariki katika haralati hizo.

Thursday, April 17, 2008

Chenge Ayaita Mabilioni Visenti!

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, amezungumzia kwa mara ya kwanza, tuhuma nzito za kumiliki kiwango kikubwa cha fedha kinachokadiriwa kuzidi dola za Marekani milioni moja katika akaunti moja nje ya nchi.
Chenge alilazimika kuzungumzia suala hilo jana muda mfupi tu baada ya kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Qatar, akitokea China alikokuwa ameongozana na Rais Jakaya Kikwete katika ziara ya kiserikali.
“Tusubiri uchunguzi ukamilike... kama ukithibitisha, hata hivyo vijisenti itajulikana vilipatikanaje,” alisema Chenge na kusababisha mshangao kwa wanahabari waliokuwa wakizungumza naye nje ya chumba cha wageni mashuhuri uwanjani hapo (VIP).
Alipoulizwa iwapo kwake yeye kiasi hicho cha zaidi ya dola milioni moja ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni moja za Kitanzania anazohusishwa nazo anaziita vijisenti, Chenge alijibu swali hilo kwa kusema: “Kila mtu ana viwango vyake.”
Akizungumza akiwa katika hali ya utulivu, tofauti kabisa na ilivyo kawaida yake ya kujibu maswali kwa mkato, Chenge alikiri kwamba tuhuma hizo dhidi yake ambazo kwa mara ya kwanza ziliandikwa katika gazeti maarufu na linaloheshimika la nchini Uingereza la The Guardian mwishoni mwa wiki iliyopita ni nzito na zilizomshtua.
Pamoja na kujaribu kujibu takriban kila swali aliloulizwa, Chenge alikataa kuelezea chochote kwa undani kuhusu kuwa na fedha hizo au njia alizozipata au iwapo kulikuwa na uhusiano wowote kati ya tuhuma hizo na kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi mwaka 2002, akisema kufanya hivyo kwa wakati huu kunaweza kuingilia uchunguzi unaofanywa na taasisi mbalimbali za dola ambazo hata hivyo hakuzitaja.
Hata hivyo alisema amekuwa kiongozi serikalini kwa muda mrefu, akishika nyadhifa tofauti, akiwa ameshika nafasi ya Uanasheria Mkuu wa Serikali kwa miaka 10, hivyo fedha alizokuwa akilipwa zilikuwa halali.
“Tuhuma za ufisadi dhidi yangu ni nzito mno… inabidi nipate muda wa kukaa na kutafakari kwanza, na ukweli wa mambo utajulikana baada ya vyombo vya dola vilivyopewa kazi ya kunichunguza kumaliza kazi yake na hapo nitakuwa na muda wa kujibu,” alisema Chenge.
Aliahidi kutoa ushirikiano wote unaotakiwa kwa taasisi zinazomchunguza kuhusiana na tuhuma hizo zinazomhusisha na umiliki wa mabilioni hayo ya fedha nje ya nchi katika Kisiwa cha Jersey.
Alisema iwapo atakutwa na hatia baada ya uchunguzi huo kukamilika, basi hatakuwa na njia nyingine zaidi ya kuwajibika.
Aidha, Chenge, mmoja wa wanasiasa ambao wamekuwa wakiandamwa tangu aliporejeshwa katika Baraza la Mawaziri katika mabadiliko ya Februari mwaka huu, alisema alikuwa akitarajia kuwasiliana na mwanasheria wake ili kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua zinazofaa.
“Nimechafuliwa jina langu sana. Sasa inabidi nipate muda wa kukaa na mwanasheria wangu Joe Mbuna, ili kufanya tathmini ya mambo yaliyoandikwa na vyombo vya habari na kuchuja yale mazuri na mabaya ili niweze kuchukua hatua za kisheria kwa mambo ambayo yameniharibia sifa zangu,” alisema Chenge.
Pamoja na hilo alisema, hata yeye anasubiri kwa hamu majibu ya uchunguzi unaofanywa na Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai ya nchini Uingereza (SFO) ambayo itachambua ukweli wa mambo, na kueleza matokeo yatakayotokana na kazi hiyo.
Katika hatua moja, Chenge alizielezea tuhuma hizo kuwa ni zenye mwelekeo wa chuki dhidi yake, akiwataka wale wanaomchukia mtu kutotumia hisia zao kumsingizia.
“Nimeshangazwa sana mambo haya, lakini kila mtu ana haki yake ya kusema na kwa hili nasema mnyonge nyongeni lakini haki yake mpeni… huwezi kumuumbia mtu tuhuma hivi hivi tu.
“Suala hapa (katika uchunguzi wa SFO) naloliona kuwa kubwa na muhimu ni hili ununuzi wa rada kutoka BAE, sasa hili la kusema kwamba Chenge ana fedha nyingi sioni kama lina nafasi, kwa vile hata mimi mwenyewe ninayo nafasi yangu na rekodi nzuri katika utendaji kazi. Nimekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka 10, naelewa mambo yangu nilivyoyafanya.”
“Napenda kuwahakikishia ndugu zangu kwamba, hii ni sehemu ya maisha kwa mtu… lakini jamani nchi hii tunaipeleka wapi?” alihoji Chenge.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama yuko tayari kujiuzulu uwaziri, ili kurejesha imani ya serikali kwa wananchi, Chenge hakukubali wala kukataa, bali alisisitiza kwamba anasubiri uchunguzi dhidi yake ukamilike kwanza kabla ya kufikia hatima yake.
“Unapouliza ndugu yangu kwamba nijiuzulu wadhifa nilionao kwa sasa, nashindwa nikujibu nini? Mimi nasubiri mchakato mzima ukamilike… nawaomba muendelee kuwa wavumilivu,” alisema Chenge.
Alipoulizwa kuwa kurudi kwake nchini mapema kunatokana na tuhuma hizo, alikanusha suala hilo na kubainisha kuwa, ratiba aliyopangiwa ilihusu kuambatana na Rais Kikwete huko China na baadaye yeye arejee nyumbanji wakati rais akielekea Marekani.
Jumamosi ya wiki iliyopita, gazeti linaloheshimika nchini Uingereza, la The Guardian liliandika kuwa katika uchunguzi huo wa SFO iligundulika akaunti moja inayohusishwa na Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni moja, zilizoko katika akaunti moja, katika Kisiwa cha Jersey.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO inamchukulia Chenge kuwa mtu anayeweza akawa shahidi muhimu katika uchunguzi mzima wa zabuni ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE ya nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO inatarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28, ambazo ni sawa na shilingi bilioni 70, mwaka 2002.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, inaaminika kwamba, uchunguzi huo wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo.
Kwa mujibu wa habari hizo, uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba, moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha hizo zinazoaminika kuwa za Waziri Chenge zilizowekwa katika akaunti moja iliyoko katika Kisiwa cha Jersey zina uhusiano wowote na zile zilizotoka katika Kampuni ya BAE System inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada hiyo kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.
The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, linaripoti kuwa, taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.
Gazeti hilo lilimkariri Waziri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Jambo la wazi linalotaka kuonekana hapa ni kwamba mimi nilipokea kwa lengo la kujinufaisha mwenyewe fedha za rushwa kutoka BAE. Huu ni uongo,” alisema Chenge.
Aidha, gazeti hilo lilimkariri Chenge akisema kuwa, wakati rada hiyo ilipokuwa ikinunuliwa yeye alihusika kwa kiwango kidogo sana katika mchakato mzima, kwani jambo hilo lilishughulikiwa na wizara nyingine na uamuzi ukaidhinishwa na Baraza la Mawaziri.
Mbali ya hilo, gazeti hilo lilimkariri mwanasheria wa Chenge anayeishi Cleveland, Ohio, nchini Marekani, J Lewis Madorsky, akikanusha kwa niaba ya mteja wake huyo, kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha zake na tuhuma zozote.
“Wakati tukitambua kuwa masuala hayo yalitokea muda mrefu uliopita, tunaweza tu tukathibitisha kuwa, tuhuma zozote za ukiukwaji wa sheria, ukiukwaji wa maadili, kutenda isivyo sawa na mambo mengine ya hivyo dhidi ya mteja wetu, ni mambo ambayo kimsingi tunayakanusha kwa nguvu kubwa,” alisema mwanasheria huyo wa Chenge.
Hata hivyo, gazeti hilo liliandika uchunguzi huo dhidi ya Chenge unamfanya yeye kuwa tu shahidi muhimu, kwani wanaielenga zaidi BAE ambayo inadaiwa ilimlipa wakala mmoja wa Tanzania mamilioni ya fedha ili kujenga ushawishi wa rada iliyokuwa ikiiuza kununuliwa.
Wakala huyo ambaye amekuwa akitajwa kwa muda mrefu na ambaye sasa anaaminika kukimbia nchini na kutafutwa na polisi wa kimataifa ni, Shailesh Vithlani.

Monday, April 14, 2008

CUF-CHENGE AKAMATWE

Chama cha Wananchi (CUF) kimetaka Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, akamatwe na kuwekwa chini ya ulinzi mara moja, wakati uchunguzi dhidi yake kuhusiana na kumiliki na akaunti yenye zaidi ya sh bilioni moja nje ya nchi, ukifanywa.

Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba, amemtaka Rais Jakaya Kikwete amsimamishe kazi Chenge haraka, ili kuwezesha uchunguzi dhidi ya waziri huyo, ambaye alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa zaidi ya muongo mmoja, kufanyika bila kuingiliwa.

Akiishadidia hoja yake ya kutaka Chenge awajibishwe, Prof Lipumba alinukuu sehemu ya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kifungu cha 29 cha sheria hiyo, ambacho kiongozi huyo wa CUF alikinuu kinasema kuwa kiongozi wa umma atahesabika kuwa amefanya kosa iwapo;
(a) atakuwa na hali ya maisha ya juu kuliko kipato chake cha sasa au awali na
(b) atakuwa anamiliki mali zisizolingana na kipato chake cha sasa au cha awali.

Kutokana na kifungu hicho, Lipumba anadai kuwa kiasi alichokutwa nacho Chenge katika akaunti yake ni kikubwa kuliko kipato chake hivyo ametenda kosa kwa mujibu wa kifungu hicho.

“Sheria na maadili ya viongozi wa umma inawataka wabunge kutoa taarifa za mali walizonazo kila mwaka. Taarifa hizi zinapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina na TAKUKURU. Ikiwa Mhe. Chenge ametoa taarifa ya akaunti zake za Jersey, je? TAKUKURU imefanya uchunguzi fedha hizo amezipataje? Kama hajatoa taarifa hizo basi amevunja sheria,” amesema Lipumba.

Lipumba ameonyesha wasi wasi wake kuhusiana na Chenge kuwa fedha hizo zote na kurejea historia yake inayoonyesha kuwa alimaliza masomo UDS< 1972 na kuajiriwa na serikali kama mwanasheria.

Alisoma shahada ya pili havard University 1975 na akarejea nchini kuendelea na kazi serikalini. Alipanda vyo hadi kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu mwanzoni mwa miaka ya tisini hadi 2005 kabla ya kuteuliwa kuwa waziri baada ya kupata ubunge huko bariadi.

Lipumba anasema kuwa ni jambo linaloshangaza kwa mtumishiw a umma kwa hali ya Tanzania kuwa na fedha zote hizo katika benki ya nje.

Gazeti la Guardian la Uingereza liliripoti mwishoni mwa wiki kuwa Cheneg alikutwa akiwa na kiasi cha dola za Marekani milioni moja katika akaunti yake iliyo katika benki moja katika kisiwa cha Jersey.

Chenge mwenyewe amekiri kuwa na kiasi hicho cha fedha katika akaungti hiyo, lakini amekanusha kuwa fedha hizo zimetokana na malipo ta rushwa kutokana na mpango wa shirika la BAE la Uingereza kuiuzia Tanzania rada ya kijeshi.

Serikali ya mseto si suluhu ya matatizo Zanzibar

INASIKITISHA kuwa watu wameanza kubishana juu ya jambo ambalo hata kama wakikubaliana na kulitekeleza kama lilivyo, haliwezi kuwa suluhu ya matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayoikabili Zanzibar hivi sasa. Achilia mbali mlolongo wa migogoro iliyosababisha kukua kwa mpasuko visiwani humo, hivi sasa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) wapo katika malumbano makubwa, kuhusiana namna ya kutekeleza makubaliano ya kuunda serikali ya mseto, kama moja ya dawa za kumaliza mpasuko huo, zilizokubaliwa katika mazungumzo yaliyofanywa na kamati iliyowakilisha vyama hivho.

Malumbano ya sasa yanayokana na msimamo wa CCM, ilioibuka katika vikao vyake vya juu vilivyofanyika hivi karibuni kijijini Butiama, mkoani Mara.

Matatizo ya Zanzibar yalianza tangu zamani lakini malumbano ya sasa, inaaminika kuwa yametokana na uamuzi wa CCM kubadilisha makubaliano ya namna ya kuundwa kwa serikali ya mseto. Wakati kwa mujibu wa rasimu moja pendekezo ni kuunda serikali hiyo mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, inadaiwa kuwa CCM imechomeka kipengele kinachopendekeza kufanyika kwa kura ya maoni kama sehemu muhimu ya kuushirikisha umma kuamua juu ya hatma ya mfumo wa utawala visiwani humo.

Lakini ieleweke kuwa tatizo hili halikuanzia na CCM kama wengi tunavyodhani na kuamini. Tatizo (hili la sasa) lilianzishwa na CUF bila ya wao wenyewe kujua kuwa wanatengeneza tatizo.

CUF ililianza tatizo hili pale ilipoamua kutangaza makubaliano ya mazungumzo peke yao bila kuwashirikisha wenzao wa CCM. Hili lilikuwa ni kosa la kiufundi na ndio maana Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alipotakiwa atoe maoni yake kuhusiana na tamko hilo la CUF, yeye alikataa akisema kuwa hilo lilikuwa ni tamko la CUF. Alijiepusha hata kusema tu kuwa yaliyotangazwa na chama hicho ni sehemu ya makubaliano waliyoyafikia, alisisitiza kuwa hilo ni tamko la CUF!

Kwa kuonyesha kuwa alikuwa anamaanisha kuwa hilo lilikuwa tamjko la CUF, Makamba aliwataka wote wanaohoji wasubiri vikao vya juu vya CCM, kwa kuwa ndivyo vitakavyotoa maamuzi kuhusiana na muafaka wa Zanzibar .

CCM ilipokaa Butiama liliibuka na pendekezo la kura ya maoni ambalo CUF imeanza kulipinga kwa nguvu zote kwa maelezo kuwa halikuwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa. Wakati nyaraka zimevuja kutoka katika vikao vya CCM zikionyesha kilichowasilishwa na Makamba kama rasimu ya makubaliano, CUF nayo imesambaza nyaraka nyingine, ikidai kuwa hiyo ndiyo rasimu halisi ya makubaliano. Katika hali kama hii ni vigumu sana kuamini ipi ni nyaraka halisi.

CUF wamelifanya jambo hilo liwe gumu kwa haraka yao ya kutaka kuipiga pini CCM na kuamua kutangaza makubaliano haraka bila kuwashirikisha wenzao. Katika kufanya hivyo, CCM sasa ina nguvu ya kuiruka CUF kimanga na kusema kuwa ilichokitangaza chama hicho ni chake chenyewe na wala CCM haihusiki nacho. Huu ni mwanzo wa mgogoro mwingine ambao nao unaongeza mpasuko ambao Rais Jakaya Kikwete alidhamiria kuumaliza kupitia mazungumzo hayo.

Lakini wapo ambao walishangilia nab ado wanaamini kuwa kuundwa kwa serikali ya mseto ndio suluhu ya matatizo ya Zanzibar . Hawa, naamini kuwa wakati walipoliangalia tatizo linaloikabili Zanzibar leo hii, walipofushwa na kile kinachotokea hivi sasa, bila kuchunguza kwa kina na sababu ya hayo yanayotokea.

Ni kweli kuwa serikali ya mseto inaweza kuwa sehemu ya dawa ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar , lakini siamini kuwa aina ya serikali iliyopendekezwa, (ambayo imefafanuliwa katika nyaraka zote mbili za rasimu ya makubaliano) inaweza kuwa ndiyo dawa yenyewe. Wala siamini kuwa serikali ya aina hiyo inaweza kuwa dawa katika mazingira yaliyopo sasa.

Mfumo wa utawala unaopendekezwa katika serikali hiyo ya mseto Zanzibar ni wa kuwa na rais atakayesaidiwa na manaibu wawili, wakati nafasi ya Waziri Kiongozi ikifutwa. Kwa mujibu wa rasimu hizo na maelezo ya wanasiasa waliohusika katika mazungumzo hayo na wasioshiriki, rais atatokana na chama kitakachoshinda uchaguzi.

Chini yake atakuwa na makamu wa kwanza, ambaye atatokana na chama kitakachoshika nafasi ya pili katika idadi ya kura katika uchaguzi. Huyu atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa rais ambaye atamsaidia katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa kila siku wa kazi za serikali. Pia huyu atakaimu nafasi ya urais wakati rais atakapokuwa nje ya nchi.

Kwa kuwa hakuna kipengele cha makamu wa rais katika katiba ya Zanzibar , imeazimiwa kuwa katika mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yatakayofanyika, maudhui ya ibara ya 47 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano yaingizwe katika katiba ya Zanzibar .

Katika utekelezaji wa kazi za serikali, haiwezekani kwa rais na makamu wa rais wa kwanza wakaw wanatekeleza sera, mipango, programu na mikakati tofauti. Ni lazima wawe wanafanya kitu kimoja. Je, inaeleweka sera zitakazokuwa zinatekelezwa ni zile za chama cha rais au makamu wake?

Pia kutakuwa na makamu wa pili wa rais ambaye atatoka katika chama cha rais. Atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi. Atakaimu urais wakati rais na makamu wa kwanza hawapo nchini.

Kama kweli haya ndiyo makubaliano, nayaona yana matatizo kadhaa ambayo yatasababisha matatizo zaidi ya yaliyopo hivi sasa iwapo yatakubaliwa kama yalivyo.

Kwanza, madaraka ya rais yatakuwa kama yalivyoainishwa katika katiba ya sasa ya Zanzibar kupitia ibara za 51, 52 na 53. Ajabu na kweli! Hivi hatujawahi kulalamika katika nchi hii kuwa katiba zetu zinawapa watawala wa juu kabisa madaraka makubwa kiasi cha kuwafanya wawe madikteta iwapo wataamua kuyatumia ipasavyo?

Iwapo katiba hiyo hiyo tuliyowahi kuilalamikia ndiyo itakayoendelea kutoa madaraka ya rais, hivi huyo makamu wake, atakayetokana na chama kitakachoshika nafasi ya pili kwa idadi ya kura, atakuwa na nafasi kweli ya kufurukuta? Au atakuwa kama kibaraka wa rais wa chama kilichoshinda uchaguzi?

Hivi rais huyu atakapoamua kuyatumia madaraka hayo dhidi ya makamu wake, nini kitamzuia? Kwa sababu atakuwa anatekeleza matakwa ya katiba. Kinachochukuliwa kama zawadi hapa ni kuwa watanzani ni mabingwa wa kutotekeleza katiba,hivyo inaaminika tu kuwa utamaduni huo utaendelea. Lakini tufahamu kuwa huu ni mchezo wa saisa.

Pili, sioni ni namna gani, katika mazingira ya Zanzibar , chama kitakachopata nafasi ya makamu wa kwanza wa rais, kiache kuhubiri sera zake na kijikite katika si tu kuhubiri, bali kutekelza pia sera za chama hasimu. Sioni urahisi wa CUF kukubali kutekelza sera za CCM au CCM kutekeleza za CUF katika mazingira yaliyopo sasa Zanzibar .

Tatu, kiongozi wa shughuli za serikali anapaswa kuwa mmoja ili kutoleta mgongano katika kinachofanywa na serikali. Katika makubaliano haya, makamu wa kwanza wa rais na yule wa pili watakuwa na jukumu la kuwa wasimamizi wa shughuli za serikali lakini maeneo mawili tofauti.

Makamu wa kwanza atakuwa akifuatilia utekelezaji wa kila siku wa kazi za serikali nje ya Baraza la Wawakilishi wakati makamu wa pili atahusika na kuangalia maslahi ya serikali katika Baraza.

Hapa naona kuna naibu mmoja anataka kufanywa kanyaboya. Na kwa kuwa makamu wa pili wa rais atatokana na chama kilichoshinda, ambacho ndicho kilichotoa rais, ninaweza kubashiri kwa uhakika kabisa kuwa makamu wa kwanza wa rais anaweza kufanywa kuwa kama kanyaboya.

Nne, kutokana na ukubwa wa Zanzibar na uwiano wake na idadi ya watu, nadhani mfumo huu utaleta serikali kubwa ambayo itakuwa mzigo mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Ikumbukwe kuwa hata katika serikali ya Muungano, Rais Kikwete alikiri wakati alipounda Baraza jipya la Mawaziri mwezi Februari kuwa kati ya vitu alivyokuwa amevifikiria katika kuunda baraza hilo , ni ukubwa wake.

Kwa hali ya Zanzibar , sioni ni kwa namna gani itaweza kuhimili serikali kubwa namna hii.

Tano, sidhani kuwa kinachotakiwa ili kumaliza mpasuko huo ni kuwapa watu madaraka. Kama lengo litakuwa kuwapa watu madaraka, hilo nalo litazaa matatizo mengine kwa sababu atakayepewa madaraka atataka kuonyesha nguvu za madaraka yake.

Katika mazingira niliyoonyesha kuwa baadhi ya viongozi wanaweza kuwa kama kanyaboya tu, ubingwa huo wa kutaka kuonyesha madaraka katika mazingira ya ukanyaboya, yatasababisha misuguano itakayopanua zaidi mpasuko.

Sita, ni suala laujumla zaidi. Ili kuleta maelewano, ninaamini kuwa kikubwa kinachotakiwa ni viongozi kuonyesha utayari na hiari (will) yao ya kufanya kile kitakachokubaliwa. Hili limekosekana tangu hapa mwanzoni na mabishano tunayoyashuhudia na tuhuma kuwa rasimu imebadilishwa, ni dalili za wazi za kukosekana kwa utayari wa viongozi.

Inatisha kuwa hilo limejitokeza katika hatua ya kufikia makubaliano kabla hatuajakubaliana na kuanza safari ya utekelezaji. Ni vigumu kufikiria hali itakuwaje watakapokubaliana na kuanza safari ya kutekeleza makubaliano hayo wakati katika hatua ya kufikia kukubaliana tu wanabishana namna hii?

Haraka ya CUF kutaka kuundwa kwa serikali ya mseto mara baada ya makubaliano hayo kusainiwa, na mbinu za CCM kutaka kuchelewesha utekelzaji wa makubaliano hayo, ni ishara nyingine ya kukosekana kwa utayari wa vyama hivyo kumaliza matatizo Zanzibar .

Saba, sioni ni namna gani serikali ya mseto itafanya kazi katika mazingira ya kutoaminiana yaliyopo Zanzibar hivi sasa. Ikimbukwe kuwa haraka ya kutaka kutekeleza kile kinachoonekana kuwa ndio suluhu, bila kuandaa mazingira yatakayofanikisha utekelezaji wa hilo lililoafikiwa, kunaweza kusababisha kushindwa kwa makubaliano hata kama kilichokuwa kimekubaliwa kweli ni dawa ya matatizo hayo.

Hili ni kama lile linalotokea Kenya hivi sasa. Baada ya Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja, watu walifanya haraka ya kushangilia kuwa hatimaye suluhu imepatikana, bila kujiuliza iwapo mahasimu hao walikuwa wamejiandaa namna gani kutachana na misimamo mikali waliyokuwa nayo saa chache tu kabla ya kufikia makubaliano?

Kinachotakiwa kuanza kufanywa Zanzibar , kama njia ya kuelekea katika suluhu ya kweli, wala si haraka ya kuunda serikali ya mseto. Pamoja na kuwa matatizo ya Zanzibar ni ya kihistoria, lakini tatizo lililopo hivi sasa linatokana na kutokubalika kwa matokeo ya chaguzi, hasa baadaya ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Tunaweza tusirudi sana kwenye historia ya zamani na kuamua kuanza kuiangalia historia ya sasa katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hili.

Kwanza itafutwe namna ambayo itahakikisha kuwa chaguzi si tu zinakuwa huru na haki, bali zionekane kuwa ni huru na haki. Tukiweza kufikia mazingira kama hayo, kila mgombea ataweza kukubaliana na matokeo ya uchaguzi hata kama atashindwa kwa kura moja.

Katika mazingira ya kuamini hivyo, hatutahitaji serikali ya mseto kwa sababu atakayeshindwa atakuwa anajua kuwa ameshindwa kwa haki, hivyo hatokuwa na sababu wala kitu cha kulalamikia. Atabaki kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi ujao.

Kukosekana kwa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki Zanzibar ni kikwazo kwa serikali ya mseto itakayoundwa. Hata kama itakubaliwa kuwa serikali ya mseto ianze sasa, mpaka utakapofika wakati wa uchaguzi, viongozi waliopo katika serikali ya mseto watakuwa wameshagongana sana kuhusiana na hili la marekebisho ya taratibu za uchaguzi kiasi kwamba hawatakuwa tena serikali moja halisi. Itakuwa ni serikali moja ambayo kila upande una mambo yake. Huo si aina ya mseto utakaoisaidia Zanzibar .

Pamoja na kuwa CCM imependekeza kura ya maoni, inapaswa kufahamu kuwa chimbuko la migogoro ya sasa ni sanduku la kura. Hivyo, kuweka mazingira ya kupiga kura kama njia ya kupata jawabu la matatizo yaliyotokana na upigaji kura, ni kurudia kosa kabla hujatafuta dawa ya kosa la awali.

Hata kama pendekezo la kura ya maoni litakubalika, inapaswa kwanza yaandaliwe mazingira ambayo yataifanya kura hiyo ionekane na wote kuwa ni huru na ya haki, kinyume na hayo, tutakuwa tunaandaa mgawanyiko mwingine.

Yapo matatizo mengi yanayoikabili Zanzibar katika nyanja mbalimbali lakini ufunguo wa hayo upo katika kukubalika kwa matokeo ya chaguzi. Hilo ndilo linapaswa kufanywa sasa kwani litazaa serikali, iwe ya mseto au vinginevyo, itakayokuwa na uhalali wa kuanza kuyashughulikia matatizo mengine bila ya kukumbana na vikwazo.

Friday, April 11, 2008

Uchaguzi wa rais DARUSO wasimamishwa

Uchaguzi wa rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (DARUSO) uliopangwa kufanyika leo umeahirishwa. Hata hivyo, hadi wakati huu sijafahamu sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huo ingawa ninaendelea kulifuatilia suala hilo na nitawajulisha baadaye.
Uchaguzi unaoendelea ni ule wa makamu wa Rais pamoja na wakuu wa mabweni.
Kampeni za uchaguzi huo zilitawaliwa na itikadi za vyama vya siasa na uzawa, huku baadhi ya wagombea wa nafasi ya rais wakituhumiwa kupokea fedha kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa kusaidia kampeni zao.
Aidha, mgombea mmoja alilalamika kufanyiwa kampeni chafu dhidi yake kwa kuwa yeye si raia wa Tanzania. Hata hivyo, mgombea huyo Mganda alisema hilo halimsumbui na ana uhakika wa kushinda kinyang’anyiro hicho.

Wednesday, April 9, 2008

Msimamo wa CUF kuleta mabadiliko Bungeni

UPO uwezekano mkubwa wa kanuni za Bunge kubadilishwa au kuongezwa nyingine, kutokana na kitendo cha wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) kususia kikao cha ufunguzi cha Bunge juzi.
Spika wa Bunge, samwel Sitta, alikiri jana kuwa kitendo hicho cha wabunge wa CUF kimebainisha kuwepo kwa kasoro katika kanuni za Bunge.
Spika alibainisha kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo, alipata ushauri wa watalaamu wa sheria. Alisema bado wanaliangalia suala hilo lakini ushauri aliokwishapatiwa unaonyesha kuwepo kwa upungufu wa kikanuni kuhusiana na suala hilo.
Alisema iwapo italazimu, kanuni zitabadilishwa au kuongezwa, ili kukabili hali kama hiyo inapojitokeza.
Aidha, Spika alisema ni lazima kanuni za Bunge ziangaliwe upya kwa sababu kwa mtazamo wake, haoni ni jinsi gani suala la mazungumzo ya CCM na CUF nje ya Bunge, yanaweza kulihusisha Bunge.
Kwa maana hiyo, alisema kuwa upo ulazima wa kuweka kanuni kwa namna ambavyo zitaweza kushughulikia tatizo kama hilo iwapo litajitokeza tena siku za usoni.
Akifafanua, alisema kuwa ipo hatari kuwa iwapo suala hilo litaachwa liendelee, hapo baadaye wabunge wa chama kingine wanaweza kutoka Bungeni kwa sababu tu wana mgogoro na chama kingine.
Upo uwezekano mkubwa kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) waliosusia vikao vya Bunge mjini Dodoma na kurejea kwenye chama chao kwa ajili ya kazi nyingine kunyimwa posho za siku ambazo hawatokuwepo Bungeni.
Hayo yalibainishwa na Spika wa Bunge, samwel Sitta, wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu hatua ya wabunge hao kuamua kuondoka baada ya juzi kususia kikao cha ufunguzi cha Bunge kutokana na kile walichokiita kuwa kukerwa kwao na kusuasua kwa mazungumzo ya kusaka suluhu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Sitta alisema jana kuwa wabunge hao hawawezi kulipwa posho kwa sababu watakachokuwa wanakifanya wakati w akikao cha Bunge, hakihusiani na shughuli rasmi za Bunge.
Wabunge wa CUF, wakiungwa mkono na wengine kutoka vyama vya upinzani, juzi walitoka nje ya ukumbi wa Bunge, muda mfupi baada ya Spika kufungua kikao cha kwanza cha Mkutano wa 11 wa Bunge hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Spika na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Miohamed, wabunge hao waliamua kuchukua hatua hiyo ili kuonyesha kutoridhishwa kwao na kusuasua kwa mazungumzo baina ya vyama hivyo.
Mazungumzo hayo yaliyochukua miezi 14 na kuelezwa kufikia hatua nzuri, yalichukua mtazamo mpya mwishoni mwa mwezi uliopita, pale CCM ilipotumia vikao vyake vya juu vilivyofanyika mkoani Mara, kubadilisha baadhi ya makubaliano, hasa yaliyohusu kuundwa kwa serikali ya mseto.
Wakati rasimu ya makubaliano hayo iliyosambazwa na CUF ikionyesha kuwa makubaliano yalikuwa ni kuundwa kwa serikali ya mseto mara moja baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, rasimu ya CCM, iliyoweasilishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu na NEC na katibu Mkuu, Yusuf Makamba, ilikuwa na pendekezo la kufanyika kwa kura ya maoni kuhusiana na uanzishwaji wa serikali ya mseto.

Tuesday, April 8, 2008

BREAKING NEWS: Wabunge wa upinzani watoka Bungeni

Bunge limeanza asubuhi hii kwa wabunge wa upinzani kutoka ndani ya Bunge wakipinga kile walichokitaja kuwa ni kusuasua kwa mazungumzo ya kusaka suluhu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Wabunge hao walisimama na kutoka baada ya kuapishwa kwa wabunge wawili wapya, ole Nangaro aliyechaguliwa hivi karibuni katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiteto na Al-Shaimaa John, mbunge wa kuteuliwa.
Baada ya kuapishwa kwa wabunge hao, wakati Spika alipomuita Waziri wa Nchi, Philip Marmo kuwasilisha hati mezani, wabunge hao walisimama na kuanza kutoka, jambo lililowafanya wabunge wengine kupiga makofi.
Hapo Spika alimsimamisha Marmo na kumtaka atulie kwanza ili ‘tukio’ hilo lipite. Walipotoka na hali kutulia, Spika alisema kuwa asubuhi, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, alikwenda nyumbani kwake na kumtaarifu kuwa wabunge wa upinzani watatoka kabla ya kipindi cha maswali na majibu kupinga kusuasua kwa mqazungumzo ya kusaka suluhu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

Monday, April 7, 2008

HOTUBA YA LIPUMBA - MUAFAKA

THE CIVIC UNITED FRONT
HOTUBA YA MWENYEKITI WA TAIFA WA CHAMA CHA WANANCHI (CUF), MHE. PROF. IBRAHIM LIPUMBA, KATIKA MKUTANO NA WAZEE, WANAWAKE NA VIJANA VIONGOZI WA CHAMA WA MKOA WA DAR ES SALAAM, KUTOA UFAFANUZI KUHUSIANA NA MAZUNGUMZO YA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KUDUMU WA MPASUKO WA KISIASA ZANZIBAR
UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE, DAR ES SALAAM
TAREHE 06 APRILI, 2008


UTANGULIZI

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima na kuweza kukutana leo hii. Naamini ataendelea kutupa baraka na mwongozo wake ili tuweze kuutekeleza wajibu wetu kama viongozi ambao ni watumishi wa Watanzania kuweza kuwapa uongozi thabiti wenye hekima na busara na utakaoiepusha nchi yetu na shari ambayo watawala waliopo madarakani hivi sasa wanaonekana kuiandaa. Nawashukuru nyinyi pia Wazee, viongozi wa Chama chetu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kina mama na vijana kwa kufika kwa wingi kuja kutusikiliza licha ya taarifa ya muda mfupi ya kufanyika kwa mkutano huu. Najua mmeacha shughuli zenu muhimu kuja kunisikiliza na kwa hilo, nasema Ahsanteni sana.

Watanzania wenzangu, sina haja ya kuwaficha, nimelazimika kuja kuzungumza nanyi ili kutumia fursa hii kuweka kumbukumbu sahihi kuhusiana na mchakato mzima wa mazungumzo kati ya Chama Cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) yenye lengo la kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar na hasa hii hali ya mtafaruku iliyopo sasa ambayo tumefikishwa na CCM. Nimeamua kufanya hivi baada ya kumsikiliza Mwenyekiti mwenzangu wa upande wa pili ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akitoa maelezo kuhusiana na mazungumzo hayo katika ukumbi huu huu wa Diamond Jubilee tarehe 2 Aprili, mwaka huu wa 2008 lakini kwa bahati mbaya maelezo hayo yakiwa yamejaa upotoshaji na ubabaishaji wa hali ya juu. Rais anatumia usanii wa kisiasa kukanusha kwamba yeye na chama chake hawafanyi usanii wa kisiasa. Nchi inapoongozwa na watu wa aina hii, Watanzania tuna kila haki na sababu ya kujiuliza iwapo kweli tuko salama hivi sasa na huko mbele tunakokwenda.
Wakati wa ufunguzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu za chama cha CUF mjini Tabora Septemba 2005 niliwatahadharisha Watanzania kuwa Mheshimiwa Kikwete ni Mtu wa mzaha mzaha, hana kauli thabiti hafai kuwa Rais na tukimchagua matokeo yake itakuwa rushwa na ufisadi itaongezeka kwa kasi, mpya na nguvu mpya. Uchambuzi wa kina wa rushwa nitaufanya katika mikutano ifuatayo leo nitachambua mazungumzo ya CCM na CUF. Hata hivyo la kuzingatia ni kuwa Mafisadi wamejikita na kujenga kambi ndani ya CCM. Hawataki demokrasia kwa sababu itawaumbua na kuwanyima nafasi ya kuendelea na ufisadi wao.

MCHAKATO WA MAZUNGUMZO

Watanzania wenzangu, mtakumbuka kuwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005, ambao kwa mara ya tatu mfululizo uliendelea kutawaliwa na wizi wa kura uliofanywa na CCM na kumuweka madarakani kwa nguvu Mheshimiwa Amani Karume kinyume na matakwa ya Wazanzibari, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lilikutana tarehe 5 Novemba, 2005 kutafakari hali mbaya ya kisiasa iliyokuwapo wakati huo ambayo ingeweza kuzaa maafa makubwa kwa nchi yetu. Wazanzibari walikuwa tayari kwa lolote baada ya kuchoshwa na wizi wa kura wa CCM katika chaguzi zote tatu, yaani 1995, 2000 na 2005. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama chetu likaamua kutumia busara na kuepusha shari kwa kuwataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla watulie na kuwapa nafasi viongozi wao kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa njia za amani.

Wengi waliomsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, wakati akilihutubia na kulizindua Bunge jipya tarehe 30 Desemba, 2005, pamoja na mambo mengine akilieleza Taifa nia yake ya kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar walidhani hiyo ilikuwa ni hoja yake mwenyewe tu. Hamkuelewa kwamba maelezo hayo ya Rais hayakuja kwa sababu ya nia yake tu bali yalitokana na mawasiliano baina ya baadhi ya wasaidizi na washauri wake wa karibu na baadhi ya viongozi wa CUF ambayo yalianza mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 kumalizika na kabla hata ya yeye kushika madaraka ya Urais. Tukakubaliana kuwa tusubiri hadi baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Muungano na tutachukua hatua za pamoja za kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

Rais alipotoa hotuba yake Bungeni, hata kama haikuwakilisha kisawa sawa mtazamo wa CUF kuhusiana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar, tuliamua kumpa ushirikiano wetu katika kutimiza ile ahadi tuliyokubaliana. Siku moja tu baada ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari na akamuandikia barua rasmi Rais Kikwete tarehe 31 Desemba, 2005 akimhakikishia ushirikiano wetu. Kuanzia hapo mazungumzo yasiyo rasmi yakawa yanafanyika kati ya baadhi ya wasaidizi na washauri wa Rais aliowaamini na baadhi ya viongozi wa CUF tuliowapa ridhaa ya kuendeleza mawasiliano hayo. Ubalozi wa nchi moja iliyo rafiki mkubwa wa Tanzania nao ukajitolea kuratibu mawasiliano hayo ili kujenga maelewano mazuri.

Jambo moja ambalo nataka niliweke wazi na Watanzania wote walielewe ni kwamba tokea hatua hizo za mwanzo kabisa, ambazo hazikuwa zikitangazwa hadharani, tulikubaliana kuwa ufumbuzi tunaoutafuta utapatikana kwa CUF kusamehe madai yake ya kutaka Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar urudiwe na badala yake itapewa nafasi ya Waziri Kiongozi na idadi kadhaa ya mawaziri kama itakavyokubaliwa. Kwa maneno mengine, makubaliano hayo yalikuwa na sura kama ile iliyokuja kujitokeza baadaye katika suluhisho la mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya ambao Rais Kikwete amejisifia sana kuwa aliweza kuumaliza kwa masaa matano tu.

Kilichokuwa kikizungumzwa katika duru hizo za awali kilikuwa ni utaratibu upi utakuja kutumika kufanikisha malengo hayo. CUF ilimweleza wazi Rais kupitia wasaidizi wake kwamba haikuwa na imani kwamba Mheshimiwa Karume na wahafidhina wenzake wa CCM Zanzibar watakubaliana na ufumbuzi huu. Naye, kupitia wasaidizi hao hao, akatuhakikishia kuwa hilo ni la ndani ya CCM na tuwaachie wao. Tulipouliza lini utaratibu huu utaanza kazi rasmi tukaambiwa tusubiri miezi sita hadi Juni 2006 pale Rais Kikwete atakapokabidhiwa uenyekiti wa Chama chake kwani atakuwa na mamlaka kamili na muhimu yatakayomuwezesha kulifanikisha suala hili.

Juni 2006 ilifika na Rais Kikwete akawa Mwenyekiti wa CCM. Tukahimiza haja ya sasa kuyawekea utaratibu wa kuyatekeleza yale tuliyokuwa tumeelewana tokea Januari 2006, tukaambiwa tumpe nafasi zaidi ya miezi sita mingine ili aweze kuweka safu vyema na kuimarisha mamlaka yake katika Chama kusudi awe na nguvu za kupitisha maamuzi mazito kama hayo. CUF kwa maslahi ya Taifa, tukakubali kusubiri hadi Desemba 2006. Ilipofika Desemba 2006, badala ya kuwa na utaratibu wa kutuelekeza kule tulikokuwa tayari tumeshaelewana kuwa ndiyo suluhisho, tukapokea tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwa imeagiza yafanyike mazungumzo kati ya CCM na CUF kwa lengo la kuanzisha siasa za maelewano Zanzibar. Pamoja na kuona hatua hiyo inaturejesha nyuma na ina lengo la kuchelewesha kufikia malengo tuliyokubaliana, CUF kwa nia njema ya kuwaamini wenzetu na hasa Rais Kikwete, tukatoa tamko kuridhia mazungumzo hayo.

Januari 17, 2007, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiambatana na Mhe. Hamad Rashid Mohamed na Mhe. Ismail Jussa, walikutana na Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Yusuf Makamba akiwa amefuatana na Mhe. Ali Ameir Mohamed na Mhe. Saleh Ramadhani Feruzi kukubaliana utaratibu wa kuendesha mazungumzo. Miongoni mwa mambo waliyokubaliana ilikuwa ni kubadilishana hadidu za rejea ambazo kila upande utaeleza matarajio yake katika mazungumzo hayo na baadaye hadidu hizo ndizo zitumike kutengeneza agenda za mazungumzo.

Katibu Mkuu wa CUF aliwasilisha hadidu za rejea zetu kwa Katibu Mkuu wa CCM kupitia barua ya tarehe 26 Januari, 2007 ambazo zilikuwa kama ifuatavyo:

Kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar:
(a) chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa; au
(b) chini ya usimamizi wa Serikali ya Mpito ya CCM na CUF
kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30, 2005 kutokuwa huru na wa haki ambako kulisababishwa na ama kutotekelezwa kikamilifu au kutotekelezwa kabisa kwa maeneo mengi ya Muafaka wa CCM na CUF wa 2001 na pia kutumika kwa nguvu kubwa na ya kupita kiasi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Vikosi vya SMZ na makundi ya vijana wa CCM ya ’Janjaweed’ katika kuwatisha wananchi wasiweze kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa uhuru na uwazi.

Kutengwa, kubaguliwa, kunyanyaswa na kukandamizwa kwa wanachama na wafuasi wa CUF walioko Zanzibar na hasa Pemba ikiwemo kunyimwa haki zote za kiraia kutokana na itikadi zao za kisiasa na kufanywa hawana haki katika nchi yao, hali inayotishia hata umoja na usalama wa nchi kwa kukuza hisia za sehemu kubwa ya wakaazi wa Pemba kuanza kufikiria hawatakiwi katika Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuendelea kuizuia na kuiwekea vikwazo CUF kufanya shughuli zake halali za kisiasa katika visiwa vya Zanzibar kama inavyopaswa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Vyama vya Siasa (Nam. 5/1992).

Askari wa Polisi na Vikosi vya SMZ pamoja na vijana wa ’Janjaweed’ waliohusika katika matukio ya uhalifu na uvunjwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wasio na hatia kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo haya.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CCM, kama ilivyo kawaida yao, akakiuka makubaliano hayo ya mapema kabisa kwa kutowasilisha hadidu zao. Hiyo ilikuwa hatua ya awali ya CCM kutokuwa wakweli katika mazungumzo haya na kama itavyokuja kudhihirika huko mbele, mara zote kutoheshimu yale yaliyokwisha kubaliwa au kujitia hamnazo kwamba hakukuwa na makubaliano kama hayo.

Badala ya kuwasilisha hadidu za rejea, CCM wakawasilisha barua ya kutaka ziteuliwe timu za watu sita kutoka kila upande na mazungumzo yaanze na kwamba wao wangetoa hadidu za rejea na mapendekezo ya agenda zao katika kikao cha kwanza cha timu hizo.

Tarehe 1 Februari, 2007, kikao cha kwanza cha timu zetu kikafanyika mjini Dodoma bila ya CCM kuwasilisha hadidu za rejea zake kama walivyokuwa wameahidi na badala yake wakasema wametumia hadidu za rejea za CUF tulizowapelekea kuandaa mapendekezo ya agenda. Baada ya mvutano wa muda, hatimaye timu yetu ilikubali yaishe na kwa pamoja kukubaliana agenda tano za mazungumzo zifuatazo:

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005: Uhalali na Taathira zake.
Usawa na Haki katika Kuendesha Siasa.
Masuala ya Utawala wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Njia za Kuimarisha Mazingira ya Maelewano na Uendeshaji wa Uchaguzi Huru na wa Haki Zanzibar.
Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.

Hata baada ya hatua hiyo, katika kila walichokieleza ni kumridhisha Mhe. Amani Karume ili asiwe na kinyongo na mazungumzo hayo, CCM ikarudi tena kutuomba upande wa CUF tukubali kuliondoa neno “Uhalali“ katika agenda ya kwanza inayohusu uchaguzi mkuu na badala yake iwe “Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na Taathira zake“. CUF kwa mara nyingine tena ikaonyesha uungwana kwa kukubali ombi hilo la CCM bila ya kipingamizi chochote. Uzuri wa haya ninayoyaeleza ni kwamba yote yamo katika Kumbukumbu za Vikao vya Kamati ya Mazungumzo ambazo zimetiwa saini na pande zote mbili.

Ni baada ya hatua hiyo, ndipo mjadala wa agenda moja baada ya nyingine ukaanza, na kila hatua makubaliano yakifikiwa. Kwa yale maeneo ambayo hayakuwa na makubaliano, ikakubaliwa kila upande ubaki na msimamo wake. Jumla ya vikao 21 vya mazungumzo vimefanyika katika kipindi cha miezi 14 tokea Januari 2007 hadi Februari 2008. Katika hatua zote hizo, kila upande ulikuwa ukitoa taarifa kwa viongozi wake wakuu na katika vikao vya maamuzi vya vyama vyetu ambavyo ni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa upande wa CUF na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa upande wa CCM.

Watanzania wenzangu, mtakumbuka kwamba mwezi Agosti mwaka jana ulizuka mtafaruku mkubwa kuhusu mazungumzo hayo pale CUF ilipobaini kwamba CCM haikuwa na nia ya dhati ya kuyakamilisha na kutekeleza yale tuliyokubaliana tokea hatua za awali kabisa za mazungumzo yasiyo rasmi. Mimi kwa niaba ya CUF nikatoa tamko tarehe 7 Agosti, 2007 kuiomba jumuiya ya kimataifa iingilie kati ili kuyanusuru mazungumzo yetu na kuiepusha nchi yetu na shari. Nilichukua hatua hiyo baada ya kuona tarehe 15 Agosti, 2007 ambayo Makatibu Wakuu wa CCM na CUF walikubaliana kuwa mazungumzo yawe yamekamilika inakaribia na hakuna dalili zote za kufanya hivyo huku CCM ikijikurupusha huku na kule kwa visingizio kemkem. Mwenyekiti mwenza wa CCM katika kamati ya mazungumzo alikuwa anadai kuwa kinyume na na uchaguzi wa mwaka 2000 na matukio ya 2001, safari hii CUF haina hoja kwa sababu hakuna mtu aliyekufa kwenye uchaguzi wa 2005. Katika jitihada za kuyanusuru mazungumzo haya nikiambatana na Mhe. James Mbatia, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, niliwasiliana na viongozi wakuu wa dini akiwemo Muadhama Kadinali Polycap Pengo wa Kanisa Katoliki, Askofu Mstaafu Elinaza Sendoro wa Kanisa la Kilutheri Tanzania na Mufti Shaaban Simba wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na kuwaomba wayaombee Mazungumzo ya CCM na CUF yanusurike na watumie nyadhifa zao kuhakikisha Rais Kikwete hayafanyii mzaha mazungumzo haya. Vile vile niliende Dodoma kuzungumza na aliyekuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara, Mhe. John Samuel Malecela na aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowasa kuwaomba watumie nyadhifa zao kuyanusuru mazungumzo.
Rais Jakaya Kikwete hatimaye akatoa tamko tarehe 14 Agosti, 2007 akiinasihi CUF ikubali kuendelea na mazungumzo hata baada ya kupita tarehe 15 Agosti iliyokuwa imekubaliwa kuwa yawe yamekwisha na akaahidi binafsi atayasimamia kuona yanafanikiwa. CUF ikaheshimu kauli ya Rais na ikakubali kuendelea na mazungumzo kwa sharti kwamba hatua zichukuliwe kuyakamilisha. Imepita miezi mingine saba baada ya ahadi hiyo ya Rais kabla ya mazungumzo hayo kukamilishwa.

Timu ya CUF iliporudi katika mazungumzo, ujumbe wa CCM ukawaeleza wenzao kuwa kwa vile makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa yanahusu mambo makubwa, ni vyema CUF ikaonyesha ustahmilivu hadi umalizike Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM hapo Novemba, 2007 ili kumruhusu Rais Kikwete kujipanga vyema na safu mpya za Chama kuweza kukabili maamuzi mazito kwa maslahi ya taifa. CUF ikawakubalia tena.

Watanzania wenzangu, ni vyema mkaelewa kuwa ustahmilivu na uungwana huo uliokuwa ukionyeshwa na CUF haukutokana na kwamba labda CUF ni dhaifu bali ni maumbile ya chama chetu, misingi yake ya ukweli na uaminifu na kujali kwake amani ya nchi yetu. Ni bahati mbaya sana kwamba CUF ilikuwa ikiyazingatia haya mbele ya CCM, chama ambacho kinaamini katika hadaa, udanganyifu, upotoshaji, ubabaishaji na usanii wa kisiasa.

Waswahili wanasema njia ya mwongo fupi. Hatimaye Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ulimalizika na mazungumzo yakaendelea na yakahitimishwa katika kikao cha tarehe 25 – 29 Februari, 2008. Tukakubaliana kuwa sasa rasimu ya makubaliano yaliyohusu agenda zote zilizowasilishwa na kujadiliwa ifikishwe kwenye vikao vya juu vya vyama vyetu ili kuidhinishwa na kisha kupanga tarehe ya kutiwa saini makubaliano na utekelezaji kuanza.

Hii ilikuwa ni hatua ya mwisho ya utaratibu (formality) tu kwa sababu kila hatua ya mazungumzo na makubaliano, viongozi wakuu wa vyama vyetu na vikao vya juu vya vyama vyetu vilikuwa vinashirikishwa na kutoa miongozo yake. Yapo mambo mengi yakiwemo hata yale yanayohusu muundo wa Serikali Shirikishi ambayo yaliwahi kufikishwa mbele ya vikao na vikao hivyo vikaagiza marekebisho yafanywe na yakafanywa. Hatua ya mwisho ilikuwa ni kuyaweka pamoja tu katika rasimu ya makubaliano ili iidhinishwe, siyo kufungua upya mjadala wa mambo yaliyokuwa yameshakubaliwa.

aik
Watanzania na ulimwengu ni mashahidi kuwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lilikutana na kuridhia makubaliano hayo tarehe 17 Machi, 2008. Timu ya CUF katika mazungumzo na CCM iliwasilisha taarifa ya mazungumzo kwa kusoma rasimu ya makubaliano ya CCM na CUF iliyokubaliwa na kupitishwa katika vikao vya kamati ya mazungumzo. Siyo kama hakukuwa na wajumbe wa Baraza Kuu la CUF ambao hawakutaka marekebisho katika makubaliano yaliyowasilishwa au waliokuwa wakiyakataa kabisa kwa kutowaamini CCM kutokana na uzoefu wa Muafaka wa Kwanza wa 1999 na Muafaka wa Pili wa 2001. Walikuwepo, lakini wajumbe wa timu ya mazungumzo ya CUF chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, na mimi nikiwa Mwenyekiti wa kikao, tulitumia busara na hekima zote kuwaeleza kwamba hatua ya sasa hairuhusu tena mabadiliko bali ni ya kuidhinisha tu kwa ajili ya kutiwa saini na utekezaji kuanza. Tulifanya hivyo kwa sababu misingi ya Chama chetu ni uungwana, ukweli, uaminifu na uadilifu.

Tulitarajia na CCM nayo kupitia vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chao ingefanya hivyo. Kwa mshangao mkubwa, wetu na hata wa watu waadilifu na waaminifu wote wa hapa Tanzania na katika Jumuiya ya Kimataifa, tumeshuhudia CCM ikiyapiga teke makubaliano hayo. Huku wakitumia makada wao waliochoka wa propaganda zilizopitwa na wakati na mabingwa wa kisasa wa siasa za kisanii maarufu kama ’spin doctors’ wamekuja na hoja mpya ya kura ya maoni na pia wakisema wamefanya mabadiliko katika baadhi ya vifungu vya makubaliano.

Katika waraka walioupeleka Butiama, ambao CUF inao nakala yake, wanasema kwa kuibua hoja ambayo haikuwepo ya kura ya maoni, CCM itakuwa imeipiku CUF kisiasa.
“Liko wazo ambalo ujumbe wetu umelipata kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Aman Abeid Karume linalohusu uzito wa makubaliano juu ya kuanzisha mustakabali mpya wa kisiasa kwa msingi wa Serikali shirikishi (power sharing arrangement) katika Zanzibar. Yeye alikuwa na fikra kwamba jambo kubwa na la kutia matumaini kama hili isingefaa maamuzi yake yakahitimishwa na viongozi katika Kamati Kuu na NEC tu. Kwa vile wadau wakuu katika hili ni wananchi wenyewe wa Zanzibar, ingekuwa bora kama suala hili likafikishwa kwao. Sisi (yaani Katibu Mkuu, ndugu Yusuf Makamba, Ndugu Ali Ameir Mohamed na Ndugu Kinguge Ngobale- Mwiru) tulivutiwa sana na pendekezo hili na tuliliunga mkono. … Kwa kukubali wazo hili CCM itakuwa imeipiku CUF katika ubunifu wa kujenga.”
Katika hali ya kawaida, waraka huu usingeweza kufikishwa mbele ya vikao bila ya Mwenyekiti wa vikao kuuona na hivyo ni wazi kuwa Rais Kikwete aliijua hoja hiyo ya kura ya maoni tokea mapema, kama si kuwa ameshiriki hata kuiandaa. Halafu eti wanataka Watanzania wawaamini kuwa hoja hiyo iliibuliwa na wajumbe wa vikao. Rais Jakaya Kikwete na CCM yake wanafanya usanii wa kisiasa katika masuala mazito yanayohusu mustakbali wa taifa letu na maisha ya wananchi wetu.


HOTUBA YA RAIS KIKWETE NA UTETEZI WAKE

Kufuatia usanii huo wa Butiama, CUF ilitoa tamko rasmi kupitia Katibu Mkuu wetu, Maalim Seif Sharif Hamad, kuzikataa hoja zote mbili za CCM, ile ya kutaka mabadiliko ya yaliyokwishakubaliwa na ile ya kura ya maoni. Katibu Mkuu wa CUF alishatoa hoja zetu za kwa nini hatuzikubali hoja hizo lakini naomba nizirejee kwa ufupi hapa:

Kuhusu hoja ya CCM kutaka marekebisho katika yaliyokubaliwa.

Kwanza, CCM haikutaja ni maeneo gani inataka yafanyiwe marekebisho. Pili, hoja hii inashangaza kwa sababu wajumbe wa Kamati ya Mazungumzo kutoka upande wa CCM walikuwa wakiwaarifu wajumbe wa Kamati kutoka upande wa CUF kwamba wao walikuwa wakiwasilisha taarifa kwa kila hatua inayofikiwa katika vikao vya chama vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa na pia kwa viongozi wao wa juu, Rais Jakaya Kikwete na Mheshimiwa Amani Karume, na kupata maelekezo na miongozo inayohitajika. Hatua hii ya mwisho ilikusudiwa kubariki makubaliano hayo yaliyokuwa yakifikiwa hatua kwa hatua na siyo kufungua mjadala mpya kupitia duru mpya ya mazungumzo.

Kuhusu hoja ya CCM makubaliano yanapaswa kuridhiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya kura ya maoni.

Muda wote wa mazungumzo ambayo yamechukua miezi 14 na yakiwa yamehusisha vikao 21, wajumbe wa Kamati ya CCM wanaoshiriki mazungumzo hawakuleta hoja hii ya kura ya maoni. Kama nilivyoeleza, pendekezo la kutaka kura ya maoni halikuwa limeibuliwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM bali lilikuwemo katika Taarifa ya Kamati ya CCM inayoshiriki mazungumzo likiwa ni pendekezo walilotaka liridhiwe na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kitendo hicho cha Kamati ya CCM kuwasilisha kitu kipya nje ya makubaliano yaliyofikiwa ni upotoshaji mkubwa wa yale yaliyokubaliwa. Iwapo pendekezo hilo lina nia njema ya kuwashirikisha wananchi, kwa nini wajumbe wa Kamati ya CCM wasiliwasilishe katika vikao vya mazungumzo na badala yake wakaamua kuliingiza kama mtego wa kisiasa wenye lengo la “kuipiku CUF”?

Kufuatia Tamko hilo la CUF, Rais Jakaya Kikwete alikuja katika ukumbi huu huu wa Diamond Jubilee na kutoa kile alichokiita ufafanuzi wa maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu Muafaka. Katika hotuba yake hiyo aliilaumu CUF kwa kile alichokiita ‘kukurupuka’ katika kutoa Tamko lake kabla ya kupata undani na msingi wa maamuzi hayo.

Inaonyesha Rais Kikwete alikuwa amesahau kauli aliyoitoa katika hotuba yake ya ufunguzi ya tarehe 28 Machi 2008 aliposema na ninanukuu
“kama ilivyo kawaida yetu, tutatoa taarifa kwa ukamilifu mwishoni mwa kikao kuhusu nini kimezungumzwa na nini kimeamuliwa.”
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Mhe. Pius Msekwa alisoma Tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu Mazungumzo ya Mwafaka baina ya CCM na CUF. Kwa kuzingatia kauli ya Mwenyekiti wa CCM katika hotuba yake ya ufunguzi hapakuwa na sababu ya kusubiri mawasiliano toka kwa Katibu Mkuu kwani ilikuwa wazi kuwa CCM hawataki kutekeleza yale tuliyokubaliana.
Katika hotuba yake ya tarehe 2 Aprili 2008 Rais Kikwete alisema kwamba amemuagiza Katibu Mkuu wa CCM kumuandikia barua Katibu Mkuu wa CUF kuyaeleza hayo kwa undani. Barua hiyo imeletwa kwetu juzi Alhamisi, tarehe 3 Aprili, 2008 ikiwa haina chochote kati ya yale yaliyoahidiwa na Rais. Kwa hakika, tamko lililosomwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Mhe. Pius Msekwa, lina maelezo yanayoeleweka kuliko barua iliyoletwa kwetu ambayo bahati nzuri si siri maana katika utaratibu mpya wa utendaji kazi wa CCM imeisambaza nakala yake kwa vyombo vya habari vyote.

Katika barua hiyo, ambayo nakala pia imeletwa kwangu, Mhe. Makamba anasema: “Sasa naomba nikuarifu rasmi kuwa Wajumbe wa Kamati ya Mazungumzo kwa upande wetu tuko tayari kukutana na Kamati yako ili kuwasilisha uamuzi na maelekezo ya Halmshauri Kuu ya Taifa kama tulivyokubaliana.“ Ndiyo kusema kuwa uamuzi na maelekezo hayo hayamo katika barua hiyo isipokuwa sasa yanatumiwa kuitega CUF kwamba ikubali kurudi katika vikao visivyokwisha na huko ndiko yatakakoelezwa. Ni wazi kuwa Rais Kikwete hakusema kweli aliposema maamuzi na maelekezo hayo yatawasilishwa katika barua ya Katibu Mkuu wa CCM kwa Katibu Mkuu wa CUF. Ni ule ule usanii wa kisiasa kwa mara nyingine tena.

Tumesikitishwa zaidi kupata taarifa kuwa katika mkutano ulioitishwa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, na Mabalozi wote wa nchi za kigeni wanaowakilisha nchi zao hapa nchini juzi Ijumaa, tarehe 4 Aprili, 2008, Waziri Membe aliamua kuwafungia ngulai mabalozi hao kwamba eti maelezo kamili ya maeneo CCM inayotaka marekebisho katika rasimu ya makubaliano pamoja na utaratibu mzima wa vipi kura ya maoni iliyopendekezwa utakuwa, umeelezwa kwa kina katika barua ya Mhe. Makamba kwa Maalim Seif. Serikali inapofikia hatua ya kuwadanganya hata mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, hatuwezi kutegemea kuwa wakweli kwa CUF na kwa Watanzania.
Rais Kikwete aliwaeleza mabalozi katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya (Sherry Party) Januari 2006 na ninanukuu:
“I will offer the authority of my office to promote, assist and facilitate an inter-party, broad dialogue on the best way to reduce the polarisation of politics in Zanzibar.” Kwa tafsiri ya kiswahili isiyo rasmi
Nitatumia madaraka ya ofisi yangu kuendeleza, kusaidia na kuwezesha mazungumzo mapana baina ya vyama ili kupata njia bora ya kupunguza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Sherry Party ya Januari 2007 aliwaeleza mabalozi:
“We are serious about the multi-stake holder dialogue on Zanzibar. We are doing the final touches to the process. Please continue to be as supportive as you have been.” Ambayo tafsiri yake ni
Tuko makini kuhusu mazungumzo baina ya wadau Zanzibar. Tuko katika kumalizia mchakato huo. Tafadhalini endeleeni kutuunga mkono katika suala hili.
Na sherry party ya mwaka huu Rais kawaeleza mabalozi kuwa
“Muafaka talks between the Civic United Front (CUF) and the ruling party, Chama cha Mapinduzi (CCM), over the situation in Zanzibar, are nearing conclusion. Hopefully, this time around we will succeed in building a firm basis for relegating divisive politics in Zanzibar as a relic of the past. I want to thank you all for being supportive of the process and for understanding its complexities, and therefore the nature of its slow pace.” Tafsiri ya kauli ya Rais ni “Mazungumzo ya Muafaka kati ya the Civic United Front (CUF) na Chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu Zanzibar yanakaribia kuhitimishwa. Ni matumaini yangu safari hii tutafaulu kujenga msingi imara wa kumaliza mpasuko wa kisiasa na kuufanya historia ya zamani. Nataka kuwashukuru nyie nyote kwa kutuunga mkono katika mchakato huu na kwa uelewa wenu wa ugumu wa tatizo lenyewe na ndiyo maana limechukua muda mrefu.”
Kinachosikitisha Rais anashindwa kuheshimu wadhifa wake na kutoa kauli nzito kwa mabalozi na viongozi wa mataifa mengine kimzaha mzaha bila ya kuwa na nia thabiti ya kutekeleza. Anayachukua mambo mazito ya nchi kama vile alivyoahidi kuwa Real Madrid watakuja kucheza mechi ya kufungua uwanja mwaka 2007 bila kujua gharama za kuwaleta Real Madrid na uwanja utakamilika lini. Bila shaka Watanzania tutamvumilia Rais wetu na usanii wake katika mambo ya mpira. Kuendeleza usanii katika mambo mazito ya Muafaka na kuwahadaa mabalozi kunahatarisha amani ya nchi yetu na kulivunjia heshima taifa letu.
Katika hotuba yake ya tarehe 2 April 2008, Rais ameeleza kuwa
“Halmashauri Kuu iliona haja ya kufanya marekebisho fulani fulani katika baadhi ya mapendekezo hasa kuhusu mapendekezo ya muundo wa Serikali Shirikishi. Shabaha ya mapendekezo hayo ni kuboresha na kuimarisha mfumo huo unaopendekezwa. Marekebisho yanapendekezwa kwenye utaratibu wa uteuzi wa Wasaidizi Wakuu wawili wa Rais wa Zanzibar na Baraza la Mawaziri. Marekebisho mengine yanahusu pendekezo la kuwepo Baraza la Usuluhishi. “
Waheshimiwa wananchi pendekezo la Muundo wa Serikali Shirikishi lilitolewa na timu ya CCM katika kamati ya mazungumzo. Timu ya CCM ilieleza mapendekezo hayo yanatokana na mashauriano waliyoyafanya na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na Makamu wake Mhe. Aman Abeid Karume. Mapendekezo ya CUF ilikuwa kugawa nyadhifa za Rais na Waziri Kiongozi kati ya vyama vitakavyokuwa vimepata kura zilizokaribiana katika kura za Rais. CUF ikatoa concession, ikaachia pendekezo lake na kulikubali pendekezo la CCM. Pendekezo la kwanza la CCM ilikuwa pawepo na Makamu mmoja wa Rais. CUF ikaridhia. Baadaye wakabadilisha kuwepo makamu wawili wa Rais. CUF tukawakubalia. Rais anaeleza kuwa NEC inataka kulifanyia marekebisho pendekezo lililoletwa na ujumbe wa CCM baada ya kupokea ushauri wake na wa Makamu wake. Sisi tuwaeleweje CCM? Kama hii siyo mbinu na usanii wa kupoteza muda na kufanya mazungumzo yasiyokwisha ni kitu gani?

Katika kutapatapa na kujitetea, Rais Kikwete amesema kwamba eti yeye ni mwanademokrasia sana na hivyo aliamua kuruhusu mjadala wa wazi kuhusu suala hilo kusudi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa watoe maoni yao kwa uwazi. Akajigamba kwamba huo ndiyo utaratibu wa CCM. Lakini akashindwa kutueleza Watanzania kuwa iwapo huo ndio utaratibu wake na wa CCM, kwa nini hakuruhusu mjadala wa wazi na wa kidemokrasia katika vikao hivyo hivyo kuhusu mafisadi wa Richmond na fedha za akaunti ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania, ambao inadaiwa ni marafiki zake wa karibu kisiasa.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliitaja mifano ya nchi kadhaa zilizotumia utaratibu wa kugawana madaraka kama njia ya kumaliza migogoro ya kisiasa kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Afrika Kusini na hata Kenya. Nilikuwa na hamu ya kumsikia akitutajia angalau mfano mmoja wa nchi iliyopiga kura ya maoni katika kuidhinisha makubaliano ya kumaliza mgogoro wa kisiasa kama ambavyo chama chake chini ya uongozi wake kimeamua kuhusu Zanzibar. Aliporudi kutoka Kenya, alijisifu sana kwamba ameweza kufanikisha kufikiwa makubaliano ya kugawana madaraka kati ya ODM na PNU, lakini hakutwambia kwa nini hakuwapa wazo la kura ya maoni ili wananchi wayaridhie makubaliano hayo.
Katika maamuzi mazito yaliyofanywa na CCM, TANU na ASP hakuna hata mara moja kura ya maoni ilitumiwa. Mwaka 1964, Tanganyika na Zanzibar ziliungana, hapakuwa na kura ya maoni. Mwaka 1965 mfumo wa vyama vingi vya siasa ulifutwa hapakuwa na kura ya maoni. Mwaka 1977 vyama vya TANU na ASP viliunganishwa, hapakuwa na kura ya maoni ya wanachama TANU na ASP. Kamati iliyounganisha vyama ikapewa kazi ya kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapakuwa na kura ya maoni. Katiba ya Zanzibar ya kwanza ya 1979 na1984 haikupigiwa kura ya maoni. Waliodai kuwepo kura ya maoni kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika miaka ya mwishoni ya 1980 waliambiwa wamechafua hali ya hewa ya kisiasa na kuwekwa kizuizuni. Tuliporejea katika mfumo wa vyama vingi hapakuwa na kura ya maoni. Katika mabadiliko ya katiba ya 11 yaliondoa nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo ambalo ndiyo msingi wa mkataba wa kimataifa wa Muungano wa dola mbili wa 1964. Jambo hili linaloidhalilisha Zanzibar lilipingwa na Wazanzibari wakiwemo wana CCM, hapakuwa na kura ya maoni.
Katiba ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano haina kipengele chochote kinachoelezea kufanya maamuzi yeyote kwa kutumia kura ya maoni. Tanzania haina sheria ya kura ya maoni. Rais hakueleza kura ya maoni itakapopigwa itakuwa ya maamuzi ya mwisho au ni ya ushauri? Kama ni ya mamuzi ya mwisho, Katiba ya Zanzibar inaeleza kuwa Baraza la Wawakilishi ndilo lenye mamlaka ya kufanya marekebisho ya katiba. Au kwa kuwa CCM wamezoea kuvunja Katiba basi suala hili haliwapi shida? Kama ni ya ushauri kwa nini kupoteza gharama kubwa ya kura ya maoni kwa maamuzi ambayo siyo ya mwisho?
Kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wanadai kushiriki kuandika katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia, CCM wamekataa kata kata. Bila kuona haya sasa wanadai kupanua demokrasia kwa kuitisha kura ya maoni kuwa ndio njia yakutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Katika ufunguzi wa Mkutano wa Butiama, Rais Kikwete alisema wamekutana Butiama kuiweka “hai kumbukumbu ya Mzee wetu hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.” Hata hivyo CCM imeendelea kudharau ushauri wa Mwalimu Nyerere alioutoa mwaka 1995 kuwa suluhisho la Zanzibar ni serikali ya umoja wa kitaifa. Rais Kikwete alimnukuu Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy, aliyesema: “mifano ya watu mashuhuri huzaa watu wa kiwango hicho”. Kuja hapa kutatupa ari ya kuishi na kutumikia taifa na watu wake kwa mfano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tulitegemea Rais ataiga alau mfano wa Mwalimu alivyokuwa akiendesha vikao vya CCM. Katika hotuba yake ya Aprili 2 inaonyesha wazi kuwa Uenyekiti wake ni dhaifu na hana dira wala msimamo. Mfano wa Uenyekiti wa Mwalimu Nyerere haujazaa Mwenyekiti wa CCM mwenye kiwango alau cha asilimia tano ya kiwango chake. Kwa Rais Kikwete kujikweza kuwa anafuata mikoba ya Mwalimu kama nukuu ya maneno ya JFK inavyolenga ni kuidhalilisha kumbu kumbu ya Baba wa Taifa.

Kwa ufupi, hotuba ya Rais Kikwete haikuwa na jipya ambalo lingetufanya CUF kufikiria upya msimamo wetu uliotolewa kupitia Katibu Mkuu wetu. Kama kuna jipya basi ni ule usanii wa Rais Kikwete wa kukanusha kufanya usanii kwa kisiasa kwa kurejea tena usanii wa kisiasa. Sasa ni rasmi kwamba Tanzania yetu inaongozwa na watu wanaosimamia usanii wa siasa na ufisadi wa uchumi. Watanzania tuna sababu na haki ya kutaka mabadiliko ili kuipatia nchi yetu uongozi makini unaohitajika kufanya maamuzi makini yanayohusu mustakbali wetu.


MUSTAKBALI WA MAKUBALIANO YETU:

Napenda nimalizie kwa kusema kuwa baada ya kumsikia Rais Jakaya Kikwete, na iwapo kweli anataka tumuamini tena kwamba dhamira yake katika kuumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar iko pale pale, basi CUF iko tayari kumsaidia kwa kukubaliana na mojawapo ya njia hizi mbili:

CCM ikubali kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya vyama vyetu viwili na endapo kweli Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho “imeyakubali kimsingi” makubaliano yaliyofikishwa kwake kama ilivyosema taarifa yake, basi ikubali kutia saini makubaliano hayo na utekelezaji wa yaliyokubaliwa uanze mara moja.

Kama kuna haja ya kutafakari maeneo hayo machache ambayo CCM inataka marekebisho, basi kwanza Rais Kikwete atembee juu ya maneno yake kwa kumuagiza Katibu Mkuu ayawasilishe kwa CUF maeneo hayo yakiwa na maelezo ya kina. Baada ya hapo, kama alivyofanya Kenya kwa kuwaweka pamoja Rais Mwai Kibaki na Mheshimiwa Raila Odinga kuhitimisha makubaliano, basi atumie kipaji chake na uwezo wake huo kuwaweka pamoja wadau wakuu wa masuala haya ambao ni Mheshimiwa Amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad kuhitimisha makubaliano hayo. Kwa njia hii, hata ile hoja inayojaribiwa kujengwa sana katika siku za karibuni kwamba viongozi wa CCM Zanzibar ndiyo kikwazo kwa kuwa hawashirikishwi katika maamuzi yanayoihusu Zanzibar na kwamba ndiyo waliokwamisha ‘nia njema’ ya Rais Kikwete itakuwa imeondoka.

Pendekezo la kufanya kiini macho cha kura ya maoni yenye lengo la kuchelewesha utiaji saini na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa HALIKUBALIKI KWA CUF.

Nawashukuru kwa kunisikiliza. Ahsanteni sana.

HAKI SAWA KWA WOTE
Dar es Salaam
06 Aprili, 2008

Sunday, April 6, 2008

Meli yazama bahari ya Hindi

MELI isiyofahamika iliyokuwa na abiria na wafanyakazi 14, imezama katika Bahari ya Hindi mwishoni mwa wiki.

Mbali na kuwa na abiria hao, meli hiyo ilikuwa na shehena ya magari matatu ya Idara ya Magereza na lita 90 za mafuta ya mitambo ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Habari zilizopatikana jana zilieleza kuwa meli hiyo ilizama usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita katika Bahari ya Hindi wakati ikiwa njiani kutokea Dar es Salaam kuelekea Mafia.

Habari hizo zinaeleza kati ya abiria hao, mwili mmoja unaosadikiwa kuwa wa nahodha wa meli hiyo umepatikana huku abiria wanane kati ya hao wakipatikana wakia hai katika eneo la Makunduchi, Zanzibar na wengine watano hado hawajulikani walipo.

Miongoni mwa abiria ambao hawajulikani waliko, ni askari magereza ambaye alikuwa akisindikiza shehena ya magari matatu ambayo ni mali ya idara hiyo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, tayari ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu na familia wa marehemu, abiria na wafanyakazi wa meli hiyo.

Aidha, Pinda ameagiza Polisi Wanamaji kwenda eneo la ajali kusaidia kuokoa watu ambao watakuwa bado wako hai na kama wameshakufa waopoe miili yao.